DORIS MOLLEL FOUNDATION YAKABIDHI MASHINE NYINGINE TATU ZA KUFUA HEWA YA OXYGEN KWA WATOTO NJITI, HOSPITAL YA WILAYA YA BUTIAMA


Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe Jumanne Sagini akipokea Mashine tatu (3) za Kufua hewa ya Oxygeni kwa watoto Njiti kutoka Taasisi ya Doris Mollel zitakazotumiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Butiama,Mkoani Mara


         Na mwandishi wetu,​

Taasisi ya Doris Mollel (DMF) imekabidhi mashine nyingine tatu za kufua hewa ya oxygen kwa Mbunge wa Jimbo la Butiama Jumanne Sagini zitakazosaidia kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa kabla ya siku zao kukamilika maarufu kwa jina ‘njiti’.

Mashine hizo zenye thamani ya Shillingi milioni 12 zitakazosaidia watoto sita kwa siku zilikabidhiwa na Mkurugenzi wa taasisis hiyo, Bi. Doris Mollel katika hosptali ya Wilaya ya Butiama.

Akizungumza katika hafla hiyo Mbunge Sagini ameishukuru taasisi hiyo na kusema kuwa Hospitali ya Wilaya ya Butiama ilikuwa na changamoto ya ukosefu wa mashine hizo na kwamba kukutana na Bi. Doris ni jambo jema kwani mashine hizo zitasaidia kuokoa maisha ya watoto njiti na ni moja ya ahadi aliyoitoa katika utekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi.

“Niliwiwa kutafuta mashine hizo baada ya kutembelea wodi za watoto njiti na kugundua kuna mapungufu ya mashine hizo. Baada ya kukutana na Bi.Doris Mollel nilimuomba na akakubali kuleta machine nne za kufua hewa ya oxygeni kwa watoto njiti”  

Mbunge Sagini aliyasema hayo leo, katika hafla ya kukabidhiwa mashine hizo kwa Hospitali ya Wilaya ya Butiama, iliyofanyika katika Hospitali hiyo mkoani Mara.

Aidha Mbunge wa Jimbo la Butiama, Mhe. Jumanne Sagini alikabidhi vifaa hivyo kwa serikali kupitia Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Mhe. Moses Kaegele ili avikabidhi vifaa tiba hivyo kwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Butiama na kutumika kuwasaidia watoto njiti.

Mkuu wa Wilaya hiyo ambaye pia ni Mgeni Rasmi wa hafla hiyo, Moses Kaegele ameshukuru Mbunge wa Jimbo la Butiama kwa jitihada alizozifanya za kuwasaidia watoto njiti wanaozaliwa katika wilaya ya Butiama na kuwaagiza wauguzi kutunza mashine hizo ili ziendele kutoa huduma kwa wananchi.

“Hii inaonyesha Serikali ya Awamu ya Sita tunapambana kuwajali wananchi wetu, niwashukuru sana Taaasisi ya DMF kwa kushirkiana na Mbunge wetu kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya watoto wanaozaliwa njiti”

Hatahivyo, Mkuu wa Wilaya ya Butiama amewaomba wananchi wa Wilaya ya Butiama hasa wakina Mama kuacha kujifungua watoto nyumbani mwao na kuwashauri kufika katika vituo vya afya pale wanapokuwa wajawazito ili waweze kupata huduma nzuri, salama na kwa wakati.

“Msijifungulie nyumbani njooni mjifungulie hospitali, mkishakuwa wajawazito fika kituo cha afya ili uweze kupata ushauri na kutengeneza mazingira sahihi ya kujifungua salama na inapotokea umepata mtoto basi huduma nzuri sasa zipo”

Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya DMF, Bi. Doris Mollel alisema mashine hizo zitasaidia watoto sita kwa siku moja na kwamba taasisi yake itaendelea kushirikiana na Halmashauri ya Butima ili kusaidia kuokoa maisha ya watoto njiti wilayani humo.

Previous Post Next Post