Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitakia kila la heri Timu ya Soka ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 ( Serengeti Girls) leo Juni 5, 2022 kwenye mchezo wa marudiano dhidi ya Cameroon ili kujihakikishia kucheza kombe la dunia.
Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo wakati akizindua mashindano ya msimu wa tatu wa mbio za marathon ya CRDB ikiwa ni masaa machache kabla ya Serengeti Girls kushuka dimbani nchini Cameroon leo Zanzibar.
Amesema watanzania wanamatumaini makubwa na wanaiombea timu hiyo ili kwa mara ya kwanza katika historia ya mchezo wa soka Tanzania ishiriki katika mashindano ya dunia ambayo yanatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini India.
Ameongeza kuwa ili kufuzu kucheza kombe la dunia Serengeti Girls imebakiza kucheza na kushinda au kutoka sare yoyote katika mechi ya leo.
Aidha amesema mafanikio haya yanapatikana sasa kutokana na mapenzi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye michezo ambapo ametoa fedha nyingi kusaidia timu zote za taifa katika michezo mbalimbali ili ziweze kufanya vizuri na kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.
" Hapa naomba nitoe shukrani na pongezi za dhati kwa Rais wetu mpendwa, kwa mapenzi makubwa na sapoti kubwa anayotoa kwenye michezo ambayo imeleta mapinduzi makubwa" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Pia amefafanua kuwa kwa mara ya kwanza Timu ya Taifa ya Soka kwa Watu wenye Ulemavu ( Tembo Warriors) inakwenda kushiriki kombe la dunia Oktoba mwaka huu nchini Uturuki.
.
Amesema tayari Serikali ametenga fedha kwa ajili ya kuzisaidia timu za taifa ambapo tayari timu zote za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa zinagharimiwa na Serikali kuanzia mwanzo wa mwaka huu.