Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango leo tarehe 17 Mei 2022 amefungua mkutano wa 31 wa pamoja wa Sayansi ulioandaliwa na Taasisi ya Taifa ya utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) unaofanyika katika kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Mkutano huo unashirikisha wataalamu na wadau mbalimbali wa sekta ya afya kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza na washiriki wa mkutano huo Amesema Tanzania inaunga mkono na kuamini katika ufanyaji wa tafiti zitakazokabiliana na changamoto za maradhi hapa nchini.
Ameongeza kuwa mkutano huo ni fursa ya aina yake kwa wanasayansi wa Tanzania kujifunza kutoka kwa kila mmoja na kuunganisha werevu na uwezo katika kupata masuluhisho ya kimsingi kwa changamoto kuu za kiafya hapa nchini.
Makamu wa Rais amesema mkutano huo una umuhimu mkubwa kutokana na kufanyika katika kipindi ambacho dunia, Tanzania ikiwemo inapitia katika changamoto mbalimbali za magonjwa kama vile Uviko 19 pamoja na magonjwa yasioambukiza.
Aidha amesema serikali imedhamiria kufikisha huduma za kiafya katika maeneo yote hapa nchini na itaendelea kushirikiana na wadau wote wakiwemo watafiti na sekta binafsi.
Halikadhalika Makamu wa Rais ameiagiza Taasisi ya Taifa ya utafiti wa magonjwa ya binadamu (NIMR) kuongeza kasi ya ufanyaji utafiti pamoja na kuzalisha chanjo na dawa bora za asili.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Ummy Mwalimu amesema wizara itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa Taasisi ya Taifa ya utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ili kuweza kutumiza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema tayari NIMR imeshiriki katika tafiti mbalimbali zinazowezesha katika utungaji wa sera na mipango katika wizara ya afya ikiwemo kuwezesha Wizara kupata uhalisia wa utoaji wa chanjo ya HPV ambayo inakinga wasichana dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.