WAZIRI MCHENGERWA AIPONGEZA WASAFI KWA KUKUZA VIPAJI VYA WASANII



Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa @mmchengerwa ameipongeza Kampuni ya Wasafi kwa kukuza sanaa ya muziki na kuzalisha ajira kwa vijana wengi hapa nchini.

Akizungumza kwenye hafla ya Usiku wa  Mahaba Ndi Ndi Ndi  siku ya wapendanao Februari 14, 2022  jijini Dar es Salaam amesema Wasafi ina mchango mkubwa katika kuibua na kukuza vipaji vya wanamuziki.




" Naomba nikuhakikishie  Serikali ipo pamoja na nyie katika kukuza sanaa " amesema Mhe.Mchengerwa

Aidha, amesema  Serikali inakwenda kushirikiana  na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wasafi mtaa kwa mtaa, kijiji kwa kijiji hadi mkoa kwa mkoa kutafuta vipaji vya wasanii lengo ni kuwashindanisha na kuwaendeleza.

Ameongeza kuwa, wizara inakwenda kuendeleza mapinduzi  ya ukuzaji wa Sanaa ili kutoa ajira zaidi kwa vijana  katika ngazi ya kitaifa na kimataifa.

Amefafanua kwamba kufanya hivyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya  kutaka kuboresha sekta hiyo ili wasanii nchini waweze kunufaika na kazi zao.

Kwa upande mwingine Mhe. Mchengerwa amesema, katika kipindi hiki sanaa inakwenda kutumika kuitangaza Tanzania kimataifa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wasafi,  Msanii nguli wa muziki wa kizazi kipya barani Afrika, Diamond Platinum ameishukuru Serikali kwa kuendelea kujenga mazingira wezeshi kwenye Sekta ya Sanaa nchini.


Previous Post Next Post