Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC Anna Henga, amesema kituo cha Sheria ha haki za Binadamu kinalaani vikali vitendo hivi vya ukiukwaji wa haki za binadamu.
"Kiufupi, vitendo hivi vya mauaji vimepelekea ukiukwaji wa haki kubwa mbili za binadamu, ambazo ni haki ya kuishi na haki ya kuwa huru na salama" amesema Anna Henga
Amesema Matukio haya ya ukatili ni mwendelezo wa matukio mbalimbali ya mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu, husani haki ya kuishi na haki ya kuwa salama, ambayo yamekuwa yakiripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo mauaji yanayotokana na wivu wa kimapenzi.
Ameongeza kuwa Ripoti ya Haki za Binadamu ya mwaka 2020 inaonyesha kuendelea kushamiri kwa vitendo mbalimbali vya ukiukwaji wa haki ya kuishi, ikiwemo matukio 32 ya wanawake kuuwawa na wenza wao, ambapo kati ya hayo matukio 23 yalihusishwa na wivu wa kimapenzi. Pia kulikuwa na matukio manne ya mauaji yaliyofanywa na maafisa vya vyombo vya dola kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Aidha amesema ukiacha matukio ya watu kuuwawa kikatili, mwezi huu pia kumeripotiwa kupotea kwa watu kadhaa pasipokuwa na taarifa za mahali walipo. Mathalani, watu watano jijini Dar es Salaam waliripotiwa kutoweka mwishoni mwa mwezi Disemba na bado haijafahamika kilichowakumba na mahala walipo.
"Tathmini iliyofanywa na LHRC imeonyesha kwamba sababu zinazochangia kutokea kwa matukio haya ya mauji na watu kujiua ni pamoja na wivu wa kimapenzi, imani za kishirikina, visasi, migogori ya mali, na afya ya akili".Amesema
Pia Mkurugenzi Anna Henga amelitakaJeshi la Polisi kuongeza nguvu ya kuwatafuta na kuwafikisha mbele ya sheria wahalifu wote waliohusika na matukio haya ya mauaji.
Aidha amewaomba Wananchi watoe taarifa kuhusiana na vitendo vya kihalifu na ukiukwaji wa haki za binadamu ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa, Hali kadhalika, viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kukemea vitendo hivi na kuwakumbusha watu na waumini wao kulinda uhai kama tunu na kuheshimu na kulinda haki za binadamu.

