Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa amezitaka Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Madini kuangalia namna ya kushirikiana kwa karibu kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini ili iendelee kuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
Naibu Waziri Kiruswa ameyasema hayo leo jijini Dodoma kwenye kikao chake na uongozi wa Tume ya Madini ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kutembelea Taasisi za Wizara ya Madini kwa ajili ya kujifunza utendaji na kubaini changamoto zilizopo na kuangaliwa namna bora ya kuzitatua.
Amesema kuwa chini ya Wizara ya Madini zipo Taasisi zilizopewa majukumu tofauti kwenye usimamizi wa Sekta ya Madini na kufafanua kuwa iangaliwe namna bora zaidi ya kushirikiana kwa karibu ili kuongeza ufanisi kwenye utendaji kazi.
"Tanzania imebarikiwa madini ya aina nyingi sana ambayo ninaamini kama Taasisi zetu zitashirikiana kwa pamoja sambamba na kushirikisha mamlaka nyingine za Serikali zinazohusika kwa namna moja au nyingine kwenye eneo la madini, mchango wa Sekta ya Madini unaweza kupaa ndani ya muda mfupi," amesisitiza Dkt. Kiruswa.
Aidha amesema kuwa, Wizara ya Madini itaendelea kutatua changamoto zinazoikabili Tume ya Madini ili kuhakikisha lengo la mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa la kufikia asilimia 10 ifikapo mwaka 2025 linafikiwa mapema.
Katika hatua nyingine ameipongeza kasi ya utendaji wa Tume ya Madini kupitia ukusanyaji wa maduhuli, uanzishwaji wa ofisi za maafisa madini wakazi wa mikoa na maafisa migodi wakazi, usimamizi wa biashara ya madini kupitia uanzishwaji wa masoko ya madini na udhibiti wa utoroshaji wa madini.
Pia ameitaka Tume ya Madini kuendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini kupitia mikutano, vyombo vya habari, vipeperushi na majarida ili kuepusha changamoto zilizopo kwenye uchimbaji wa madini ikiwa ni pamoja na migogoro ya ardhi.
Naye Kamishna wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga sambamba na kupongeza utendaji wa Tume ya Madini amehimiza suala la usimamizi bora wa usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.



