WAZIRI MKUU AZITAKA SHERIA ZA BARABARA ZITEKELEZWE BILA UPENDELEO



 







Na Lilian Ekonga, Dar es salaam


WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amevitaka vyombo vinavyosimamia usalama barabarani vitekeleze sheria hizo bila upendeleo kwani tabia ya kuogopana na kuoneana aibu imechangia baadhi ya watu kukwepa wajibu wakati wengine wakibebeshwa mzigo wa sheria.


Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Novemba 26, 2025) wakati akifungua Maadhimisho ya Kimataifa ya Wiki ya Usafiri Endelevu Ardhini katika ukumbi wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.


Amesema kuwa haitakuwa uungwana kuona baadhi ya watu wakilipa adhabu papo hapo wanapokosea ilhali wengine wakiachwa kupita bila kuchukuliwa hatua.





"Yeyote atakayevunja sheria akamatwe na hatua zichukuliwe kwa usawa. Huyu mmoja anavunja sheria anakamatwa, analipa. Huyu mwingine anavunja mbele yake anaachwa. Kama una haraka, toka mapema zaidi si kufidia kwa kuvunja sheria."


Amewaonya baadhi ya viongozi na madereva wa Serikali ambao wanaelewa sheria vizuri lakini bado wanazikiuka kwa makusudi. "Ni muhimu kuwasaidia watumiaji wa vyombo vya usafiri kama bodaboda na bajaji ambao kwa sehemu kubwa wanaweza kuwa hawazielewi sheria kikamilifu, badala ya kuwaadhibu kwa upendeleo."


 Mwigulu amesisitiza umuhimu wa kuwapa Watanzania wote heshima na kuhakikisha sheria zilizowekwa zinatekelezwa kwa maslahi ya wote na kuongeza kuwa endapo zipo sheria ngumu kutekelezeka, basi zibadilishwe ili kila Mtanzania anufaike.


Ameviagiza vyombo vya usimamizi wa sheria vihakikishe kuwa watumiaji wote wa vyombo vya usafiri wanazingatia usimamizi wa sheria na kuchukua hatua kwa yoyote anayevunja sheria akamatwe na kuchukuliwa hatua bila kuonewa aibu


"Inaudhi mtu amebeba mgonjwa anafuata sheria, halafu mwingine anapita tu anavunja sheria, hapati adhabu. Mlalahoi akivunja sheria anapata adhabu, tunawapa kazi watekeleza sheria kuwaomba radhi watu waliovunja sheria. Naelekeza kila mtu afuate sheria, uwe wa serikalini ama uwe binafsi, tumeweka sheria, zifuatwe kama zilivyo.





Kwa upande wake Waziri wa Uchukuzi Prof.Mbarawa amesema Maonesho haya yanaonesha wazi dhamira ya nchi yetu katika kupunguza uchafuzi wa mazingira, kuongeza ufanisi na kuhimiza matumizi ya nishati mbadala kwenye mifumo yetu ya usafirishaji.


Aidha, amewahimiza wananchi kufika Mnazi Mmoja kujifunza kuhusu teknolojia mpya, miradi ya usafiri endelevu, huduma za wizara, na fursa zinazotolewa na taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi na kuwataka wawekezaji binafsi kuchangamkia fursa sasa kuwekeza kwenye miradi ya uchukuzi.


Mkurugenzi Mkuu wa Latra CPA Habibu Suluo amesema mamlaka itaendelea kusimamia matumizi ya mifumo ya kidijitali na kuhimiza matumizi ya nishati safi kama njia ya kuongeza ufanisi wa Sekta ya Uchukuzi na kutunza mazingira






Maonesho haya yaliyoanza tarehe 24 November, 2025 yenye kaulimbiu ya " Nishati Safi na Ubunifu katika Usafirishaji" yataendelea hadi tarehe 29 Novemba 2025.

Previous Post Next Post