Na Lilian Ekonga, Dar es salaam
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema kuwa sekta ya viwanda na biashara ni muhimili muhimu katika uchumi wa Tanzania kutokana na mchango wake mkubwa katika Pato la Taifa, mapato ya ndani, pamoja na kuongezeka kwa mauzo ya nje.
Ameyasema hayo alipotembelea Ofisi ya Tume ya Ushindani (FCC),kwa lengo la kuona utendaji na utekelezaji wa majukumu ya tume hiyo, Novemba 24, 2025, Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa mikakati ya Serikali inalenga kuendeleza na kuongeza wigo wa viwanda chini, kwani kupitia viwanda kutaimarisha ajira, kukua kwa mapato ya ndani na kupanuka kwa mauzo ya nje
Aidha amesema. FCC ni taasisi muhimu kwa mustakabali wa Taifa kutokana na majukumu yake ya kudhibiti ushindani kibiashara, kulinda haki za walaji, kudhibiti bidhaa feki, kutoa elimu kwa umma na kusimamia mienendo ya makampuni makubwa, ikiwemo kushughulikia masuala ya muunganiko wa makampuni ili kuhakikisha ushindani unadumishwa kwa manufaa ya nchi.
Waziri Kapinga amepongeza tume hiyo kwa jitihada zake, akibainisha kuwa matokeo chanya yanayoonekana katika jamii ni uthibitisho wa kazi kubwa inayofanywa na FCC katika kulinda maslahi ya wananchi.
“Ziara ya leo inalenga kuimarisha misingi iliyopo ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi. Tunafahamu Watanzania wanatutegemea; wao ndiyo walaji na wateja wetu. Hivyo kikao hiki kinalenga kuboresha namna tunavyotekeleza majukumu na kuimarisha mifumo ya kupokea mrejesho kutoka kwao,” alisema Waziri Kapinga.
Ameongeza kuwa mazungumzo yao yamegusia pia mikakati ya kuimarisha mapambano dhidi ya bidhaa feki, suala ambalo bado ni changamoto kubwa nchini, pamoja na kuongeza ubunifu na ushirikiano na sekta binafsi ili kuboresha zaidi mazingira ya biashara.
Kadhalika, Waziri Kapinga amesema kuwa kwa kuwa dunia ya biashara inabadilika kwa kasi, ni muhimu kwa FCC na Wizara kuweka mikakati madhubuti inayowezesha taasisi zao kuendana na mabadiliko hayo na kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Khadija Ngasongwa, alisema kupitia marekebisho ya sheria yaliyopitishwa na Bunge, tume imeweka vifungu maalum vinavyolinda na kutetea haki za mlaji, hasa pale anapopata usumbufu au madhara kutokana na bidhaa zisizokidhi viwango.
Amesema tume imeweka mfumo unaozingatia falsafa tatu—kurekebisha (repair), kubadilisha (replace) na kurejesha fedha (refund)—kwa bidhaa zinazolalamikiwa. “Endapo mlaji atashindwa kupata suluhu dhidi ya mtoa huduma, FCC huingilia kati kwa utaratibu wa kimahakama. Tumetenga siku maalum za kusikiliza malalamiko katika ngazi ya kamati ili kuhakikisha mlaji anasikilizwa moja kwa moja,” alieleza.
Ngasongwa amesema falsafa hiyo imeongeza ufanisi wa tume katika kushughulikia malalamiko ya walaji na kutoa matumaini mapya kwa wananchi. “Tumejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake, na tumefarijika kuona mfumo huu ukileta matokeo chanya kwa Watanzania,” alisema.






