Na mwandishi wetu
Benki ya CRDB leo imezindua rasmi maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja ya mwaka 2025 katika hafla maalum iliyofanyika kwenye tawi la Dar Village, jijini Dar es Salaam. Maadhimisho hayo yanafanyika chini ya kaulimbiu ya kimataifa “Mission Possible”, ambayo Benki hiyo imeitafsiri kama “Mkakati Unaowezekana”.
Akiongoza hafla hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, alisema kaulimbiu ya mwaka huu inaakisi safari ya mafanikio ya miaka 30 ya benki hiyo – safari iliyojengwa juu ya misingi ya uthubutu, ubunifu, na mahusiano ya karibu na wateja.
“Tulipoanza mwaka 1996, wengi hawakuamini kama tungeweza kushindana na mabenki makubwa ya kimataifa. Lakini leo hii, CRDB ni benki inayoongoza Tanzania na kinara wa huduma za kifedha katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati,” alisema Raballa.
Raballa alieleza kuwa mafanikio ya benki hiyo yamechochewa na maamuzi sahihi ya kimkakati, ambayo yamewezesha upanuzi wake kimataifa hadi Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), pamoja na kuanzishwa kwa taasisi mpya kama CRDB Insurance na CRDB Bank Foundation.
Aliongeza kuwa kupitia huduma bunifu kama CRDB Wakala na SimBanking, Benki imekuwa chombo muhimu cha kujumuisha Watanzania wengi zaidi katika mifumo rasmi ya kifedha.
“Leo hii mkulima wa parachichi kutoka Madeke, Njombe anaweza kupata huduma kupitia AMCOS yake inayotumia CRDB Wakala; mwalimu wa Malinyi anaweza kufuatilia mshahara wake kupitia SimBanking bila kulazimika kusafiri; na mama mjasiriamali wa Mwanjelwa anaweza kupata mtaji kupitia programu ya IMBEJU bila dhamana yoyote. Hii ndiyo maana halisi ya Mission Possible,” alisisitiza Raballa.
Akizungumzia maendeleo ya kiteknolojia, Raballa alisema Benki hiyo hivi karibuni imekamilisha uboreshaji mkubwa wa mfumo wake mkuu wa kibenki kwa kuanzisha mfumo mpya wa Temenos Transact (T24), unaoendana na viwango vya kimataifa.
“Mfumo huu umepanua uwezo wetu wa ubunifu, kuongeza kasi na usalama wa huduma, na umetuwezesha pia kujiandaa kuingia kwenye masoko mapya kama Dubai,” aliongeza.
Raballa alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba radhi wateja waliokumbwa na changamoto wakati wa kipindi cha mpito kuelekea mfumo mpya, akiahidi kuwa huduma zote zimerudi katika ubora wake na benki itaendelea kujitahidi zaidi katika utoaji wa huduma bora.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja, Bi. Yolanda Uriyo, alisema Benki ya CRDB inaamini kuwa utoaji wa huduma bora si jambo la msimu, bali ni utamaduni wa kila siku.
“Wiki ya Huduma kwa Wateja ni muda maalum wa kuwashukuru wateja wetu kwa imani yao, pamoja na kuwapongeza wafanyakazi wetu kwa kazi nzuri wanayoifanya kila siku,” alisema Uriyo.
Alibainisha kuwa shughuli mbalimbali zimepangwa kufanyika wiki nzima, zikiwemo mikutano na wateja, semina, na kampeni za kusikiliza maoni kupitia majukwaa ya kidijitali.
Naye mgeni maalum wa hafla hiyo, Bw. Hashim Lema, ambaye alimwakilisha wateja wa Benki, alitoa pongezi kwa CRDB kwa kuwa mfano wa mafanikio ya kizalendo.
“Huduma za CRDB zimetuwezesha wafanyabiashara, wakulima, wanafunzi, na wastaafu kutimiza ndoto zetu. Tunajivunia kuwa sehemu ya Mission Possible,” alisema.