DKT. JINGU: WANAWAKE VIONGOZI AFRIKA CHUKUENI HATUA ZA KWELI ZA UONGOZI





Na Lilian Ekonga Dar es Salaam, Oktoba 5, 2025 – 


Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu, amewataka viongozi wanawake chipukizi kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika kuchukua hatua madhubuti na kuleta mabadiliko halisi katika safari zao za uongozi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Tano wa Uongozi wa Wanawake ulioandaliwa na Taasis ya Uongozi (Uongozi Institute), Dkt. Jingu alisisitiza umuhimu wa kutumia maarifa waliyonayo kuleta ushawishi na matokeo chanya katika jamii.


“Msikae tu na kuandika madokezo. Tafuteni mtu ambaye safari yake inawatia moyo. Mhamasishe mtu mwingine. Shiriki mawazo yenu. Na muhimu zaidi, jiwekeni wakfu kwa hatua moja—kikwazo kimoja mtakachokivunja, daraja moja mtakalojenga kwa ajili ya wengine,” amesema Dkt. Jingu.


Mkutano huo uliwakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Afrika Kusini, Rwanda, Gambia, Zambia, Nigeria na Liberia, ambao wanatoka katika sekta za umma, biashara, elimu na asasi za kiraia.


Kaulimbiu ya mkutano huo mwaka huu ni “Mchango wa Uongozi wa Wanawake Afrika”, ikichota msukumo kutoka falsafa ya Kiafrika ya Ubuntu inayosema “Mimi ni kwa sababu sisi sote tupo.”


Dkt. Jingu alieleza kuwa uongozi wa kweli haupaswi kuishia kuvunja vizingiti tu, bali pia kuunda nafasi kwa wengine, kubadilisha mifumo, na kuongozwa kwa huruma na ushirikiano.


Aidha, alimtaja Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kama mfano bora wa uongozi wa mwanamke barani Afrika, huku akieleza kuwa changamoto kama upendeleo usiojitambua, mzigo wa majukumu ya kazi na familia, pamoja na ukosefu wa kujiamini bado ni vikwazo kwa wanawake wengi.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Uongozi Institute, Kadari Singo, alieleza kuwa taasisi hiyo imezindua Mpango Maalum wa Wanawake Katika Uongozi, ambao umelenga kuongeza uwakilishi wa wanawake katika nafasi za juu za kisiasa, kiuchumi na kibiashara.



“Mpango huu umetokana na wito wa mara kwa mara wa kuchukua hatua. Umebuniwa kulingana na safari za kipekee za uongozi za wanawake,” amesema Singo.


Aliongeza kuwa washiriki wa mpango huo walichaguliwa kwa ushindani mkubwa na tayari wamekamilisha mafunzo ya awali.


Akinukuu takwimu za kimataifa, Singo alisema wanawake wanashikilia asilimia 22 ya viti vya bunge duniani na asilimia 21 ya nafasi za uwaziri, nyingi zikiwa katika sekta za kijamii.


Naye Afisa wa Mpango kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Alessandro Pisani, alieleza kuwa mkutano huo ni hatua muhimu katika juhudi za kuingiza usawa wa kijinsia katika ajenda ya maendeleo Afrika. Alisisitiza ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya, Serikali ya Tanzania na Shirika la UN Women katika kubomoa vikwazo vya kimfumo dhidi ya uongozi wa wanawake.



Mwakilishi wa UN Women Tanzania, Katherine Gifford, alielezea mpango huo kuwa ni hitaji la maendeleo, akisisitiza kuwa juhudi za kuwawezesha wanawake zinapaswa kuenda mbali zaidi ya uwakilishi wa majina tu.


Kwa upande wake, Balozi wa Finland nchini Tanzania, Theresa Sitting, alizungumzia changamoto za kijamii kama vile matarajio ya kulea familia katika umri mdogo kwa wanawake, akibainisha kuwa uongozi si nafasi tu, bali ni safari ya kujitambua na kustahimili changamoto.



“Uongozi ni kujiamini, siyo cheo pekee. Tusikubali kuogopa kuanguka. Tukishaanguka, tuamke na tujaribu tena,” amesema


Mkutano huo umeendelea kuwa jukwaa la kujadili nafasi ya wanawake katika uongozi barani Afrika na kutengeneza njia ya pamoja ya kufikia usawa wa kijinsia.

Previous Post Next Post