WANUFAIKA WA BIMA WAONGEZEKA HADI KUFIKIA MILIONI 25.9 -TIRA




Na Lilian Ekonga Dar es Salaam, Agosti 18, 2025 

 Idadi ya Watanzania wanaonufaika na huduma za bima imeongezeka kutoka watu milioni 14 mwaka 2021 hadi kufikia milioni 25.9 mwaka huu, kwa mujibu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).


Kamishna wa TIRA, Dkt. Baghayo Saqware, ametoa taarifa hiyo leo jijini Dar es Salaam katika kikao kazi kati ya wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), akisema kuwa mafanikio hayo ni matokeo ya utekelezaji madhubuti wa sera pamoja na elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa bima.


 “Mafanikio haya yamechangiwa na utekelezaji wa sera bora chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na juhudi za uelimishaji kwa kutumia mifumo mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari,” amesema Dkt. Saqware.




Aidha, thamani ya mali na mitaji katika soko la bima imepanda kutoka Sh trilioni 1.2 mwaka 2021 hadi trilioni 2.3 mwaka 2025.

Kamishna huyo pia amebainisha ongezeko la watoa huduma za bima kutoka 993 mwaka 2021 hadi 2,425 mwaka huu, ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa aina mpya za huduma kama bima ya kidijitali, afya na mtawanyo. Idadi ya kampuni za bima pia imeongezeka kutoka 32 hadi 35 katika kipindi hicho.

Katika hatua nyingine, Serikali kupitia TIRA imefanikiwa kutunga Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote ya mwaka 2023, inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi wote. Sheria hiyo pia inaiweka NHIF chini ya usimamizi wa TIRA.

Dkt. Saqware pia ametaja mafanikio ya maboresho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2022, inayolazimisha miradi yote ya Serikali kukatiwa bima, pamoja na kuanzishwa kwa consortium za bima za kilimo (kampuni 15) na mafuta na gesi (kampuni 22).

Ameongeza kuwa TIRA imepiga hatua kubwa katika matumizi ya TEHAMA kwa kuunganisha mifumo yake na taasisi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Mamlaka ya Mapato (TRA), LATRA, TASAC na NIDA, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha huduma kwa wananchi.


“Lengo letu ni kuunganisha taasisi zaidi ya 30 Tanzania Bara na Visiwani ili wananchi wapate huduma kwa haraka na ufanisi,” amesema.

 



Previous Post Next Post