Na Lilian Ekonga...
Dar es Salaam, Agosti 18, 2025 – Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amewataka viongozi wa vyama vya siasa nchini kuhakikisha kampeni za Uchaguzi Mkuu wa 2025 zinafanyika kwa nidhamu na heshima, bila kutumia lugha za matusi, kashfa, au vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumza katika mafunzo kuhusu Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa viongozi wa kitaifa wa vyama vya siasa, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, Jaji Mutungi alisisitiza kuwa vyama vina wajibu mkubwa wa kulinda misingi ya amani iliyoasisiwa na waasisi wa taifa.
“Nendeni mkafanye kampeni za kistaarabu mkiwanadi wagombea wenu. Jiepusheni na lugha za matusi, kashfa, uchochezi au vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa taifa letu,” alisema Jaji Mutungi.
Aliongeza kuwa uchaguzi si mwisho wa siasa wala maendeleo, hivyo viongozi wanapaswa kuzingatia kuwa kuna maisha baada ya uchaguzi, na kuhakikisha urithi wa amani unarithiwa na vizazi vijavyo.
Aidha, aliwaonya viongozi wasikubali kupotoshwa na taarifa zinazozagaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu uchaguzi, na kusisitiza kuwa uchaguzi utafanyika kama ulivyopangwa.
“Mtaambiwa uchaguzi haupo, msikate tamaa. Uchaguzi upo, na nyie ndio wakala wa kwanza wa kuhakikisha unakuwa huru na wa haki,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sehemu ya Ruzuku kutoka Ofisi ya Msajili, CPA Edmund Mugasha, alisema kuwa sheria ya Gharama za Uchaguzi ya Mwaka 2010 (Sura ya 278) inawataka wagombea na vyama vyote kuweka wazi mapato na matumizi ya kampeni zao.
“Sheria hii inalenga kuhakikisha fedha zinatoka kwenye vyanzo halali na matumizi yanafanyika kwa mujibu wa sheria, ili kulinda usawa wa kidemokrasia,” alisema Mugasha.
Alihimiza vyama kuwahamasisha wagombea wao kuhusu umuhimu wa uwazi wa kifedha, akisisitiza kuwa udhibiti wa gharama ni msingi wa uchaguzi huru na wa haki.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatibu, alikumbusha historia ya kasoro zilizojitokeza tangu kuanzishwa kwa sheria hiyo mwaka 2010, ambapo baadhi ya wagombea waliwasilisha taarifa za kughushi wakidhani wangerejeshewa fedha.
“Wengine walijaza gharama hewa na kutengeneza risiti bandia. Sheria hii haifanyi kazi hivyo, leo tunatarajia kupata elimu ya kutosha ili kuepuka makosa ya awali,” alisema Khatibu.