Na mwandishi wetu.....
Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria imeweka wazi umuhimu wa kutambua na kusimamia ipasavyo utajiri na maliasili za nchi, kwa mujibu wa sheria zilizopitishwa mwaka 2017.
Akizungumza na SatMedia, katika maonesho ya 49 kimataifa ya Biashara (Sabasaba) Wakili wa Serikali na Mkurugenzi wa Kitengo cha Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Maliasili za Nchi, Bi. Neema Mwanga amesema kuwa kabla ya mwaka huo, Tanzania haikuwa na utaratibu wa pamoja wa kutambua na kusimamia rasilimali za nchi kama sehemu ya utajiri wa taifa.
“Utajiri na maliasili, kama inavyoelezwa kwenye sheria zetu, ni pamoja na rasilimali zote za asili ambazo nchi yetu imejaaliwa kuwa nazo. Hapa tunazungumzia gesi asilia, milima, mabonde, tambarare, volkano, na kila kilicho ndani ya ardhi kwa asili yake – vyote hivyo ni utajiri,” amesema Bi. Mwanga.
Amefafanua kuwa baadhi ya rasilimali hizo kama mawe, hata bila kuongezewa thamani, tayari ni utajiri, huku nyingine zinahitaji kuboreshwa ili kuleta tija zaidi kwa taifa. Vilevile, ameeleza kuwa rasilimali kama wanyamapori, samaki, na ardhi yenyewe ni sehemu ya utajiri wa nchi.
Kwa mujibu wa Bi. Mwanga, hatua ya msingi ilichukuliwa mwaka 2017 kupitia kutungwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusu Uangalizi wa Utajiri wa Asili na Maliasili za Nchi – Sura ya 449, ambayo imeweka misingi ya kuhakikisha kuwa uvunaji na matumizi ya rasilimali hizo una manufaa kwa wananchi wote.
“Wizara ya Katiba na Sheria haijishughulishi moja kwa moja na uvunaji wa rasilimali hizo. Kwa mfano, madini yanavunwa chini ya Wizara ya Madini. Lakini sisi jukumu letu ni kuhakikisha kuwa zipo sheria, mifumo, na misingi madhubuti ya kuhakikisha wananchi wananufaika – iwe kupitia ajira, elimu, au teknolojia,” amesema.
Aidha, Bi. Mwanga ametaja kuwa pamoja na sheria ya Sura ya 449, kuna pia sheria nyingine zinazohusu majadiliano na usimamizi wa mikataba ya rasilimali, zenye lengo la kulinda maslahi ya taifa na kuhakikisha kuwa mikataba ya kimataifa inayoingiwa na nchi inaleta faida halisi kwa wananchi wa Tanzania.
Kwa ujumla, amesisitiza kuwa dhamira ya serikali ni kuhakikisha kuwa utajiri mkubwa uliopo nchini unaendelezwa kwa njia endelevu na shirikishi, huku kila Mtanzania akinufaika.

