ASA YAWAHAMASISHA WAKULIMA MATUMIZI SAHIHI YA MBEGU BORA KATIKA MAONESHO YA SABASABA






Na mwandishi wetu...

Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) umeendelea kushiriki kikamilifu katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), ambapo unatoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mbegu bora ili kuongeza tija katika kilimo.

Akizungumza katika banda la ASA, Afisa Masoko wa ASA, Wakirya John, alisema kuwa lengo kuu la ushiriki wao ni kuwaelimisha wakulima kuhusu majukumu ya ASA pamoja na huduma wanazotoa kwa kushirikiana na serikali.

“Sisi kama ASA tumepewa jukumu na serikali la kuzalisha na kusambaza mbegu bora kwa bei elekezi ili kumuwezesha mkulima kupata mavuno mengi na yenye ubora,” alisema Wakirya.

Alibainisha kuwa ASA inatoa mbegu bora za mazao mbalimbali ikiwemo nafaka, ufuta, alizeti, mboga mboga, jamii ya mikunde pamoja na miche ya matunda, ambapo wakulima wanaweza kupata elimu na mbegu hizo kwa gharama nafuu moja kwa moja katika banda lao.

“Tunawakaribisha wakulima na wadau wote wa kilimo kutembelea banda letu lililopo katika eneo la Wizara ya Kilimo. Tunatoa elimu ya moja kwa moja kuhusu matumizi ya mbegu bora na faida zake kwa mkulima,” aliongeza.




Wakirya alieleza kuwa tangu maonesho yafunguliwe rasmi tarehe 28 Juni 2025, kumekuwa na muitikio mkubwa kutoka kwa wananchi, hasa wakulima waliotumia mbegu za ASA mwaka jana, ambao walirejea kutoa ushuhuda wa mafanikio waliyopata kutokana na mavuno bora.

“Wapo wakulima waliotembelea banda letu mwaka jana, walichukua mbegu zetu, sasa wamepita tena kutoa ushuhuda wa jinsi matumizi sahihi ya mbegu bora yalivyowawezesha kuongeza kipato,” alisema.

Aidha, ASA imelenga si tu kutoa elimu bali pia kujenga mahusiano ya karibu na taasisi mbalimbali na wadau wa sekta ya kilimo, huku ikisisitiza dhamira ya kuwafikia wakulima wa mijini na vijijini bila ubaguzi.

“Tunaamini mafanikio ya mkulima yanatokana na elimu sahihi ya kilimo, na sisi kama ASA tupo mstari wa mbele kuhakikisha kila mkulima anapata maarifa hayo popote alipo,” alisisitiza Wakirya.

Maonesho ya Sabasaba yanatarajiwa kuendelea hadi Julai 13, 2025, na ASA inatarajia kutoa huduma kwa maelfu zaidi ya wakulima na wadau wa kilimo nchini.




Previous Post Next Post