TANESCO YAZINDUA KAMPENI YA KUHAMASISHA ULIPAJI WA MADENI KWA HIARI




Na Mwandishi wetu....


Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limezindua rasmi kampeni maalumu ya kitaifa yenye lengo la kuhamasisha ulipaji wa madeni kwa wateja wa malipo ya baada na kuimarisha ulinzi wa miundombinu ya umeme nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 19 Juni 2025, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO, Bi Irine Gowelle, amesema kuwa kampeni hiyo inayojulikana kwa jina la “Lipa Deni, Linda Miundombinu, Tukuhudumie” inalenga kuboresha huduma ya umeme kwa wananchi kwa kuhakikisha malipo ya madeni na matumizi sahihi ya miundombinu ya umeme.

“Kampeni hii imebeba kaulimbiu ya ‘Huduma endelevu huanza na wewe’ ikihamasisha ulipaji wa madeni kwa hiari kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria, pamoja na kutoa motisha kwa wateja wanaolipa kwa wakati,” amesema Bi Gowelle.


Amefafanua kuwa kampeni hiyo itahusisha pia ukaguzi wa mita kwa wateja wa LUKU, hususan kwa wale wanaotumia mita zilizoshukiwa kuchezewa au kutoonekana katika mfumo wa TANESCO. Zoezi hilo litaenda sambamba na utoaji elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya Shirika ili kuhakikisha huduma ya umeme inapatikana kwa uhakika.

“Tunahamasisha ulinzi shirikishi wa miundombinu kwa kushirikiana na wananchi katika kutoa taarifa kuhusu vitendo vya kihalifu kama vile wizi wa umeme, uharibifu au wizi wa vifaa vya umeme. Hili ni jukumu letu sote kama wananchi na wadau wa maendeleo,” aliongeza.

Bi Gowelle ametoa wito kwa wateja wote wanaodaiwa kulipa madeni yao mapema ili kuepuka usumbufu wa kukatiwa umeme na kuathiri shughuli zao. Kadhalika, TANESCO inahimiza wananchi kushirikiana na vyombo vya usalama kutoa taarifa za uhalifu ili kudhibiti uharibifu wa miundombinu na kulinda rasilimali za taifa.

Kampeni hii ni sehemu ya mikakati ya Shirika hilo katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora, endelevu na salama ya umeme kwa Watanzania wote.
Previous Post Next Post