Na Lilian Ekonga........
Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira bora na wezeshi kwa wakunga nchini, ikitambua mchango mkubwa wanaoutoa hasa katika mazingira magumu na kazi ngumu wanayoifanya ya kuwahudumia mama na watoto wakati wa kujifungua.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi wa Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Ahmed Mohamed, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali katika kuboresha sekta ya afya, hususan huduma za uzazi salama, ambapo wakunga wamebainika kuwa nguzo muhimu ya mafanikio hayo.
Kwa mujibu wa viongozi wa sekta ya afya, serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wakunga wanapata mafunzo ya mara kwa mara, wanapewa vitendea kazi vya kisasa pamoja na kuwezeshwa kufanya kazi katika mazingira salama na yenye staha, hasa wakati wanapokabiliana na changamoto kama vile milipuko ya magojwa hatarishi.
Hayo yanajiri wakati Tanzania inajiandaa kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wakunga ambapo Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania, Bi. Beatrice Mwilike, amesema maadhimisho hayo yataambatana na mafunzo maalum kwa wakunga, lengo likiwa ni kuwaongezea weledi katika maeneo mbalimbali ya utoaji wa huduma.
"Maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika mkoani shinyanga katika viwanja vya Fire, kuanzia tarehe 4 hadi 5 Mei 2025, huku huduma za afya za bure zitapatikana kwa wananchi, huku mabanda ya maonyesho ya kazi mbalimbali za wakunga yakionyesha mchango wao katika jamii, siku ya kilele tarehe 5 Mei kutakuwa na matembezi ya wakunga kuonyesha kazi zao na kuhamasisha umma kuhusu umuhimu wa huduma za uzazi" amesema Mwilike.
Mwilike ameongeza kuwa Sambamba hayo watatoa mafunzo ya kupunguza utokaji wa dami kwa wingi baada ya mama kujifungua ambalo limekuwa tatizo kubwa linaongeza kwa kina mama wanapojifungua alikadhalika na kufanya warsha ya namna ya kumuhudumia mtoto anapozaliwa.
Kwa upande wake, Mkunga kutoka kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu, Said Abdallah, ameeleza hali halisi wanayokumbana nayo katika mazingira ya kazi na umuhimu wa kuendelea kupewa msaada wa kitaalamu na vifaa.
Sunday Rwebangira Mratibu Miradi Shirika la idadi ya watu Duniani UNFPA Tanzania amesema Shirika la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA) limeahidi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine katika kuwawezesha wakunga nchini, ili kuimarisha huduma za afya ya uzazi na kuhakikisha usalama wa mama na mtoto.