Na Mwandishi Wetu...............
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Ally Gugu amefungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo Watendaji wa Ofisi na Madawati ya kushughulikia Mrejesho kutoka Wizara hiyo na Vyombo vyake vya Usalama yakiwa na lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi kwa Wizara na Vyombo vyake vya Usalama
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Mafunzo hayo leo Januari 15, 2025 jijini Dodoma Katibu Mkuu amesema kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha kila malalamiko, maoni, mapendekezo na pongezi zinazotolewa na wananchi zinashughulikiwa kwa wakati na kwa uwazi.
"Ushughulikiaji wa Mrejesho si suala la kushughulikia malalamiko pekee bali ni kujenga uhusiano mzuri kati ya Serikali na wananchi kwa kuhakikisha maoni yao yanasikilizwa na yanapewa uzito unaostahili," Amesema Gugu
Ameongeza kuwa Serikali imeandaa Mwongozo wa Ushughulikiaji wa Mrejesho wa Wananchi wa mwaka 2023 ili kuwezesha Taasisi zote za Umma kuwa na mfumo thabiti wa kushughulikia mrejesho wa wananchi kwa weledi na uwajibikaji.
Aidha, Katibu Mkuu amesisitiza umuhimu wa watendaji hao kutumia maarifa watakayoyapata katika Mafunzo hayo kuboresha huduma wanazotoa kwa wananchi ili kujenga imani na kuimarisha utawala bora.
Kwa upande wake Msajili wa Jumuiya za Kiraiya, Emanuel Kihampa ameishukuru Serikali kwa kuandaa mafunzo ya kuwajengea uwezo watendaji wa Madawati ya kushughulikia Mrejesho amesema kuwa mafunzo hayo yatawaweka katika nafasi nzuri ya kutekeleza kwa vitendo dhana ya 4R ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
"Kupitia mafunzo haya Wizara itaweza kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi pamoja na kuimarisha taswira chanya ya Wizara ya Mambo ya Ndani ili kuendelea kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu" Amesema Kihampa