KUANZIA JANUARI 2025, VIVUKO VITAKUWA VINASUBIRIA ABIRIA, SEA TAX KUONGEZWA DAR: BASHUNGWA




Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali kupitia Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) kwa kushirikiana Kampuni ya Azam Marine zinaendelea kuboresha utoaji wa huduma za usafiri wa vivuko katika eneo la Magogoni – Kigamboni jijini Dar es Salaam ambapo kufikia mwezi Januari 2025 vitaongezwa vivuko vidogo (sea tax) kufikia sita (6) ambapo ushirikiano huo utaondoa changamoto kwa wananchi kusubiri vivuko kwa muda mrefu. 

Bashungwa ameeleza hayo leo Novemba 19, 2024 Dar es salaam wakati akikagua huduma za usafiri wa vivuko ambapo ameeleza kutokana na changamoto iliyopo sasa, kuanzia kesho (Novemba 20,2024) Azam Marine kwa kutumia sea tax itaongeza muda wa kutoa huduma kulingana na ilivyokuwa awali ili kupunguza msongamano wakati wa asubuhi na jioni. 

“Nimeelekeza  kufika Disemba 31, 2024 majengo ya kisasa ya abiria yawe yamekamilika na tuingie mwaka mpya wa 2025 tukiwa na Sea tax za Azam sita, hilo lina maanisha kuanzia Januari 01, 2025 vivuko vitakuwa vinasubiria abiria badala ya abiria kusubiria vivuko ambapo mwananchi atasubiri kivuko kwa dakika zisizozidi 3”, amesema Bashungwa. 




Bashungwa ameeleza kuwa uboreshaji wa utoaji wa huduma za usafiri wa vivuko unaenda sambamba na ujenzi wa majengo ya abiria ya kisasa na uboreshaji wa majengo yaliyokuwepo ambapo ameagiza kazi hiyo ikamilike ifikapo Disemba 31, 2024.

Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na kampuni ya Azam Marine kwa ajili ya kuboresha huduma ya usafiri wa vivuko kwa wananchi wa Mafia ili kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji na kuchochea shughuli ya Utalii na Uchumi kwa wananchi wa mkoa wa Pwani. 

Katika hatua nyingine, Bashungwa amekagua ukarabati mkubwa wa Kivuko cha MV Kigamboni katika karakana ya Songoro Marine ambapo amebainisha kuwa Serikali tayari imemlipa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 kwa ajili ya ukarabati wa vivuko mbalimbali nchini, hivyo amemtaka Mkandarasi huyo kukamilisha ukarabati kwa kivuko hicho kwa wakati ili kiweze kutoa huduma kwa wananchi wa Kigamboni.

Wakati huo, Bashungwa ametoa onyo kali kwa wavuvi wanaofanya shughuli zao katika njia za vivuko na kupelekea nyavu kunasa kwenye vivuko na kusababisha hitilafu ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
 
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TEMESA, Lazaro Kilahala ameeleza ushirikiano na kampuni ya Azam Marine umeongeza utoaji  huduma ya usafirishaji kwa wananchi wakati ukarabati wa Vivuko vya MV Kigamboni na MV Magogoni ukiendelea na kufafanua kuwa changamoto iliyojitokeza imetokana na sea tax moja kupata hitilafu.

Naye, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni Azam Marine, Abubakar Aziz ameeleza kuwa mpaka sasa ujenzi wa majengo ya abiria kwa upande wa Magogoni umefikia asilimia 70 na upande wa Kigamboni umefikia asilimia 60, majengo hayo yatahusisha ofisi za mawakala wa mauzo ya tiketi kwa njia ya kielektroniki.




Previous Post Next Post