Na Joyce Ndunguru, Morogoro
Katika kuunga mkono jitihada za Serikali katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori nchini, Kampuni ya Bushman Safari Trackers iliyopo Mkoani Morogoro imetoa msaada wa pikipiki sita (6) zenye thamani ya shilingi za kitanzania Millioni Kumi na tano (15,000,000) Kwa Askari wa Uhifadhi wa TAWA kwa ajili ya kusaidia shughuli za doria katika Pori la Akiba Maswa.
Akimkabidhi Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange msaada huo katika Ofisi za Makao Makuu ya TAWA zilizopo Mkoani Morogoro Oktoba 31,2024, Captain Willness Minja kwa niaba ya Kampuni ya Bushman amesema wamekabidhi vitendea kazi hivyo kwa ajili ya kusaidia shughuli za doria katika Pori la Akiba Maswa wao kama miongoni mwa wadau wakubwa wa uhifadhi katika hifadhi hiyo.
Kwa upande wake, Kaimu Naibu Kamishna Kabange ameishukuru Kampuni ya Bushman kwa ufadhili huo ambao unalenga kuimarisha usimamizi wa shughuli za uhifadhi na ulinzi wa rasilimali za wanyamapori.
"Tunashukuru sana wawekezaji wetu kwa msaada huu na vitendea kazi hivi vitaenda kuongeza nguvu na utarahisha ufanyaji kazi wa doria, vilevile tunawaomba Bushman tuendelee kushirikiana zaidi katika ulinzi wa rasilimali za wanyamapori" amesema Naibu Kamishna Kabange.
Aidha, ameongeza kusema kuwa TAWA inatambua mchango wa wawekezaji na itaendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha rasilimali za wanyamapori zinalindwa kikamilifu.