ZAIDI YA WATU 4000 WAMEHUDUMIWA NA KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA YA MAMA SAMIA


Na Humphrey Msechu, Dodoma 

KAMPENI ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia mpaka sasa imehudumia wananchi zaidi ya 4000 katika mikoa saba hapa nchini, waliokuwa na changamoto mbalimbali za kisheria katika jamii.

Aidha toka Agosti Mosi, 2024 maonesho yalipoanza ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi mkoani Dodoma kampeni hiyo imefanikiwa  kusikiliza migogoro 26.

Kaimu Mkurugenzi Kitengo cha Huduma cha Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ester Msambazi amesema hayo katika maonesho hayo yanayoendelea jijini Dodoma.

Msambazi ambaye pia ni Msajili wa Mashirika yanayotoa huduma ya msaada wa kisheria, ametaja huduma zinazotolewa kuwa ni ushauri wa kisheria pamoja na kuwaandalia wananchi nyaraka za kisheria ili waweze kuwasilisha mahakamani.

Pia kutoa elimu kwa makundi yanayowatembelea wakiwemo wanafunzi, wanawake wa vikundi vya kiuchumi, kusikiliza migogoro ya mtu mmoja mmoja ambapo toka maonesho yameanza wameshasikiliza migogoro 26.

"Migogoro hiyo inahusu ardhi, mirathi, ndoa, matunzo ya watoto na migogoro mingine. Kwa hiyo tunatoa rai kwa wananchi wa Dodoma na mikoa jirani wafike katika banda wapate elimu ya msaada wa kisheria," amesema.

Amesema huduma hizo za kisheria zinagharimiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Previous Post Next Post