SHULE YA SEKONDARI HASNUU MAKAME YAITIKIA AGIZO LA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA




📌 Mwalimu Mkuu aeleza namna Nishati Safi ya Kupikia ilivyookoa nusu ya gharama

📌 Aeleza athari zilizopatikana wakati wakitumka nishati isiyo safi

Moja ya maagizo ya Serikali kuelekea katika safari matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini ni taasisi zikiwemo shule kuachana na matumizi  ya nishati zisizo safi na salama kama kuni na mkaa wa asili na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi.

Shule ya Sekondari ya Hasnuu Makame, iliyopo Mkoa wa Kusini Unguja Visiwani Zanzibar imeanza kutekeleza agizo hilo kwa vitendo ambapo sasa wanafunzi wanafurahia chakula kilichopikwa kwa kutumia nishati safi.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Bw. Mohammed Ally anasema matumizi ya kuni shuleni hapo  yaligharimu kiasi kikubwa cha fedha na pia kuathiri mwenendo wa masomo kwa wanafunzi. 

"Tulilazimika kupeleka wanafunzi hospitali mara kwa mara na maranyingi matatizo makubwa yanakuwa ni ukosefu wa maji kunakosababishwa na kutokula kutokana na chakula kuwa na moshi wa kuni." Anasema Bw. Ally

Anatanabaisha kuwa, wakati Shule hiyo ikianzishwa ilikuwa na Wanafunzi 110 ambapo ilikuwa ikitumia kiasi cha shilingi 650,000/- kila mwezi kwa ajili ya kununua kuni.

Anasema hivi sasa Shule ya Hasnuu ina wanafunzi 471 huku ikitumia shilingi 778,600 kwa miezi miwili kwa ajili ya kununua gesi na kwamba kwa idadi ya wanafunzi ya sasa endapo wangetumia kuni kupikia gharama zingekuwa kubwa zaidi.

Bw. Ally anaeleza kuwa gharama nyingine zilizookolewa kutokana na matumizi ya nishati safi ni gharama za ukarabati wa jiko zilizotokana na kuchakaa kwa sababu ya moshi pamoja na gharama za maziwa kwa Wapishi.
Previous Post Next Post