MAMLAKA YA MADAWA YA KULEVYA NCHINI YAZIDI KUTOA ELIMU KWA WANANCHI KUHUSU MIRUNGI NA BANGI


Na Humphrey Msechu, Dodoma

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, inawakaribisha wananchi kwa ajili ya kupata elimu kuhusu dawa za kulevya aina ya mirungi na bangi ambazo zimekuwa zikilimwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Kamishna Msaidizi wa Kinga na Huduma za Jamii katika Mamlaka hiyo, Moza Makumbuli ametoa mwaliko huo katika maonesho ya Wakulima, Wafugaji na Wavuvi  yanayoendelea Viwanja vya Nziguni, Dodoma.

Amesema mbali na bangi na mirungi pia wapo kwa ajili ya kutoa elimu kuhusu dawa za kulevya za aina nyingine mbalimbali ikiwemo cocaine na heroine.

Amesema katika maonesho hayo mamlaka hiyo inahusika kwa kuwa kuna baadhi ya dawa za kulevya zinatokana na kilimo haramu zinazolimwa hapa nchini zikiwiwemo bangi na mirungi.

"Tumekuja na mbangi wenyewe. Tunapinga kilimo cha bangi. Hivyo tumeleta sampuli za dawa mbalimbali za kulevya ili watu wazitambue na kutoa taarifa," amesema.

Amesema kwa Tanzania bangi inalimwa katika maeneo mengi, inapelekwa mpaka nje ya nchi, na kutaja maeneo yanayoongoza kwa kilimo hicho kuwa ni Mara, Arusha, Tabora na Pwani.

"Same mkoani Kilimanjaro ni makao makuu ya kuzalisha mirungi. Nasi hatutachoka kuelimisha wananchi kuwa kilimo hicho ni haramu," amesema.
Previous Post Next Post