LHRC: BAJETI YA SERIKALI YA MWAKA 2024/25 NI MATUMIZI YA KAWAIDA KULIKO MAENDELEO


Na Lilian Ekonga, Dar es salaam

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kuwa makadirio ya mapendekezo ya bajeti ya Serikali kwa mwaka 2024/2025 yamekuwa ni ya matumizi ya kawaida zaidi kuliko maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati akitoa maoni ya LHRC kuhusiana na bajeti hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Wakili Fulgence Masawe amesema bajeti ya serikali kwa asilimia 70 ni matumizi ya kawaida huku asilimia 30 ndio ya maendeleo.

Amesema hali hiyo inaonyesha wazi kuwa wananchi wasitegeme maendeleo makubwa au miradi mipya ya maendeleo kwani bajeti hiyo ni ya matumizi ya kawaida na kulipana mishahara pamoja na madeni.

“Matumizi mengine ya kawaida yamekuwa ni ya anasa ambayo ni pamoja na magari ya kifahari na watendaji wakuu wan chi kuishi Dar es Salaam muda mwingi kuliko Dodoma hali inayosababisha kuhudumia miji mikuu miwili ambapo ni gharama kubwa.



“Kuna haja ya kuangalia ukubwa wa serikali, kuongeza cheo cha Naibu Waziri Mkuu kinaongeza gharama kwa serikali, wizara zimekuwa na nyingi kwa sasa zina manaibu Waziri na naibu katibu ,” amesema


Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kituo hicho, Wakili Fulgence Masawe
Amesema kwa mujibu wa bajeti hiyo vyanzo vya mapato vimeendelea kuwa vile vile huku wanaochangia bajeti kwa njia ya kodi ni wananchi wachache.

“Hata vyanzo vya mapato kama vilevi sio endeleevu kwani watanzania wakiamua kubadilisha mfumo wa maisha na kuacha kunywa na kuvuta ina maana nchi itashindwaa kujiendeleza.

“Kuna haja ya serikali kubuni vyanzo vipya vya mapato, mfano mchango wa halmashauri kwenye bajeti yetu ni mdogo sana, halmashauri nazo zimeshindwa kubuni vyanzo vipya mfano kupima ardhi kwa wingi na kumilikisha wananchi ili kupata kodi ya ardhi,” amesema
Aidha Massawe amesema kumekuwa na uhaba wa fedha za kigeni nchini na kwamba kinachosababisha uhaba huo ni uwiano kati ya bidhaa zinazouzwa nje na zinazoingizwa.

“Serikali inatakiwa kuwa na mkakati wa kufufua na kuhamasisha uzalishaji wa mazao ya biashara kama kahawa, pamba, mkonge na korosho,” amesema

Amesema Serikali lazima iwe na mkakati wa kujenga mazingira rafiki na kuhamasisha wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza nchini

Kuhusu deni la Taifa, Massawe amesema kukua kwa deni la Taifa hadi kufikia Trilioni 91.7 kunaashiria kwamba ukali wa maisha unaweza kuongezeka na utasababishwa na ulipwaji wa deni hilo.

Amesema ni maoni yao kuwa ni muhimu kwa serikali kupunguza gharama za uendeshaji ikiwemo posho, maisha ya kifahari na magari ya gharama kubwa ambayo yanaweza kuwa na mbadala wake.

Massawe amesema pendekezo la kuweka tozo kwenye gesi inayotumika kuendesha mitambo, magari na bajaji linarudisha nyuma lengo namba 13 la Malengo Endelevu ya Dunia.

“Lengo hilo limeweka malengo madogo ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuweka mipango ya kisera ili kupambana na mabadiliko ya tabianchi, tunafahamu nishati ya gesi na umeme ni moja ya nishati zenye madhara ya chini kwenye kuzalisha hewa ya ukaa ikilinganishwa na mafuta ya petroli na dizeli,” amesema

Hata hivyo amesema LHRC inapendekeza kupunguza kodi ya ongezeko la thamani kwenye bidhaa zote zenye uhitaji mkubwa kwenye matumizi ya nyumbani kama vile bidhaa za chakula ili kupunguza ukali wa maisha.
Previous Post Next Post