WANAFUNZI WA KIKE SHULE YA SEKONDARI LUMVE WAPEWA BAISKELI KUKABILIANA NA CHANGAMOTO YA UMBALI WA SHULE


Na Mwandishi Wetu, Magu

Wanafunzi wa kike wa shule ya Sekondari Lumve iliyopo Kata ya Bujora Wilayani Magu wamemshukuru Diwani wa kata ya Bujora Mh. Bunyanya John kwa kushirikiana na mfadhili Ndugu. Jefta Kishosha ambao wamekabidhi baiskeli 54 kwa wanafunzi wa kike wa shule hiyo ili kuwapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu kwenda shule.


Wakizungumza wakati wakipokea baiskeli hizo wanafunzi wa shule hiyo akiwemo Ester John na Hellen Mmasi wameeleza kuwa baiskeli hizo zitawasaidia kupunguza changamoto ya kutembea umbali mrefu kwenda shule ambao umekua ukidumaza kiwango cha elimu na kuwafanya wakutane na madhara mbalimbali ikiwemo kuchelewa shule.


"Baiskeli hizi zitatusaidia kwa kiasi kikubwa kuepuka changamoto kwani tutawahi shuleni na kufaulu kwa kufanya vyema kwenye masomo yetu kwani tutawahi shule na kupata muda wa kujisomea"

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Bujora Mh. Bunyanya John amemshukuru Ndugu Kishosha kwa kutoa baiskeli hizo na kubainishia kuwa zitasaidia kupunguza changamoto ya umbali na kurahisisha usafiri kwa wanafunzi na kuwaepusha vishawishi vya kurubuniwa njiani na watu kama bodaboda kwa kuwapa lifti na kuwafanyia ukatili wa kingono.


Amesema changamoto nyingine wanazokutana nazo wanafunzi ni pamoja na kutokua na matokeo mazuri, na kuvamiwa na wanyama wakali kwani wengi huamka mapema sana kwaajili ya kuwahi shule hivyo kupatikana kwa baiskeli hizo kutasaidia kuongezeka kwa ufaulu.

Naye mfadhili aliyetoa baiskeli hizo ndugu Jefta Kishosha alitoa wito kwa wazazi kua mstari wa mbele kwa kuzitunza baiskeli hizo na kuacha kuzitumia katika matumizi tofauti ya ilivyokusudiwa ikiwemo kubebea maji na mizigo mbalimbali.







Previous Post Next Post