TANZANIA YASHIKA NAFASI YA NNE AFRIKA KWENYE USALAMA WA ANGA


Na Mwandishi Wetu, Dar

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania imefanikiwa kushika nafasi ya nne barani Afrika kwenye masuala ya usalama wa anga kwa kupata alama 86.7 ikitanguliwa na Nigeria, Kenya na Ivory Coast katika ukaguzi uliofanyika Mei, 2023.

Waziri Mkuu amesema hayo leo Jumatatu, Oktoba 30, 2023 wakati akifungua maadhimisho ya miaka 20 ya TCAA kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


“Kwenye ukaguzi mwingine wa uwezo wa nchi kiusalama uliofanywa na Shirika la ICAO, viwanja vya ndege vya KIA, Zanzibar na JNIA Dar es Salaam vilikaguliwa na kupata alama 86.7. Hatua hiyo, imewezesha nchi yetu kushika nafasi ya nne Barani Afrika ikitanguliwa na nchi za Nigeria, Kenya na Ivory Coast. Huu ni ushahidi tosha kwamba uwezo wa nchi yetu katika kudhibiti usalama wa anga unaendelea kuimarika,” amesema.


Waziri Mkuu ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi huo, amesema Tanzania imeweza kuongeza uwezo wa udhibiti wa sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini kwa viwango vya kimataifa.

“Kupitia kaguzi za Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), sekta ndogo ya usafiri wa anga nchini, imeongeza uwezo kutoka asilimia 37.8 mwaka 2013 hadi asilimia 69.04 mwaka 2019. Kutokana na ufaulu huo, ICAO imetoa ufadhili wa dola za Marekani milioni moja ambazo zilitumika kwenye mradi wa kuendelea kuboresha uwezo wa usimamizi wa anga letu.”


Ametaja mafanikio mengine kuwa ni ongezeko la mchango wa sekta ya uchukuzi katika Pato la Taifa huku akibainisha kuwa katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo, sekta hiyo ilichangia asilimia 8.2 ya pato la Taifa kwa mwaka 2022.


Akitoa mfano wa ongezeko hilo katika kipindi cha miaka 10, Waziri Mkuu amesema: “Jitihada za Serikali zimechangia ongezeka la abiria na mizigo inayosafirishwa ndani na nje ya nchi ambapo idadi ya abiria imeongezeka kutoka 1,662,452 mwaka 2003 hadi abiria 4,614,380 mwaka 2023. Aidha, mizigo imeongezeka kutoka tani 33,255 mwaka 2003 hadi tani 55,806.20 mwaka 2023.”
Previous Post Next Post