TANZANIA NA DR CONGO ZAKUTANA KUJADILI KUHUSU KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA KUKUZA BIASHARA NA UCHUMI


Na Mwandishi Wetu,

Waziri wa Fedha. Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mhe. Ekila Libombo, kuhusu mipango ya kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji ili kukuza biashara na uchumi wa nchi hizo mbili.,,

Mazunguzo hayo yamefanyika mjini Kinshara, Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, kando ya mkutano wa Kamati ya Mawaziri wa Fedha na Uwekezaji wa jopo la mapitio ya uchumi mpana katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Katika mazungumzo yake, Mhe. Dkt Nchemba alitaja maeneo kadhaa ya ushirikiano ikiwemo, Tanzania kupatiwa kibali cha ndege za abiria za Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanza kufanya safari kati ya mataifa hayo mawili ili kuwezesha biashara ya usafirishaji wa abiria na mizigo.


“Ujenzi wa miundombinu ya barabara upande wa Mashariki mwa DRC, kuanzia maeneo ya jiji la Lubumbashi, Moba hadi kufika Bandari ya Kalemie, na ujenzi wa reli ya SGR itakayounganisha Nchi za Burundi na DRC kutokea Uvinza-Tanzania hadi Kindu nchini DRC kupitia Musongati na Gitega nchini Burundi ni miradi muhimu” Alisema Dkt. Nchemba

Dkt. Nchemba alisema kuwa maombi ya DRC ya kupatiwa eneo la Bandari Kavu kwa ajili ya kuhifadhia mizigo ya nchi hiyo linafanyiwa kazi na Tanzania, kupitia Wizara husika ya Ujenzi na Uchukuzi, na taarifa itatolewa ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo kupitia Bandari ya Dar es Salaam. 

Aidha, Dkt. Nchemba alisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa amani na usalama katika maeneo yenye mapigano hususan eneo la Mashariki mwa DRC ili miundombinu inayotarajiwa kujengwa iweze kuwa na manufaa kwa watumiaji na hatimaye malengo yaliyokusudiwa ya kuimarisha biashara na huduma za usafiri kwa wananchi yaweze kufikiwa.

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi wa DRC, Mhe. Likombo alisema kuwa nchi yake kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Anga inaendelea kufanya uchambuzi wa maombi ya Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Alisema DRC imekubali kugharamia ujenzi wa kipande cha Reli kutoka Uvira hadi Kindu ambapo kwa sasa upembuzi yakinifu unafanyika ili kubaini gharama nzima ya ujenzi wa mradi huo.
Previous Post Next Post