77 EXPO VILLAGE YAWAKUTANISHA WADAU SEKTA YA MADINI


SEKTA ya Madini imeendelea kukuwa kutokana na uwekaji wa mazingira wezeshi ya uwekezaji uliochagizwa na miongozo na sera thabiti chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa mstari wa mbele kuitangaza sekta ya madini kimataifa na kuvutia wawekezaji.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa akifungua Jukwaa la Madini Tanzania, Sabasaba Expo Village 2023 jukwaa lililoandaliwa na kampuni ya TanzaKwanza kwa kushirikiana na Mamlaka ya Biashara Tanzania (TANTRADE.)

Amesema, marekebisho ya sheria zinazosimamia sekta ya madini pamoja na ushirikishwaji wa wadau wa sekta hiyo vimechangia ukuaji wa sekta hiyo ambayo ukuaji wake umefikia asilimia 7.75 kwa mwaka na kuchangia Fedha za kigeni Dola za kimarekani milioni 5,505 kwa mwaka.

Dkt. Kiruswa amesema kuwa, Serikali itaendelea kusaidia na kuweka mazingira bora na wezeshi ya biashara ili kuhakikisha kuwa wawekezaji na wafanyabiashara wanafanikiwa na kuchangia katika ukuaji wa sekta ya Madini na uchumi wetu.

Kuhusiana kuanzishwa kwa Jukwaa la 77 Expo Village amesema, ni moja ya dhamira ya kukuza Sekta ya Madini na kuvutia uwekezaji nchini na ameipongeza kampuni ya TanzaKwanza kwa kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya sita katika kukuza na kujenga uchumi imara wa Nchi na watanzania kwa ujumla.

"Kupitia jukwaa hili, tunawapa fursa wadau wote walio kwenye mnyororo wa thamani ya madini kuonesha ujuzi na uwezo wao, kutafuta masoko mapya, na kujenga uhusiano na wadau wa ndani na nje ya nchi," amesema Dkt. Kiruswa.

Awali Mkurugenzi mwenza wa kampuni ya TanzaKwanza Francis Daud amesema, jukwaa la 77 Expo Village ni bidhaa mpya katika maonesho hayo na wamewakutanisha wadau wa sekta mbalimbali pamoja na taasisi zake na kujadili fursa na changamoto katika kuboresha sekta za kimkakati.

Amesema, kupitia jukwaa hilo Serikali imekutana na wadau wanaowawekea mazingira wezeshi ya uwekezaji na kujadili namna ya kuendelea kushirikiana na kujenga uchumi wa Taifa.

"Tutaendelea kuboresha jukwaa hili, mwaka huu tumezikutanisha Wizara ya madini na taasisi zake na wizara ya TEHAMA na taasisi zake umekuwa wakati mzuri na tunaamini kupitia jukwaa hili tutaboresha zaidi huduma zetu kwa manufaa ya Taifa." Amesema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewashukuru wadau wa Sekta ya Madini kwa kushiriki kikamilifu katika jukwaa hilo la Madini. Amesema Serikali kupitia Sekta ya Madini itaendelea kutengeneza mazingira rafiki ya biashara na uwekezaji nchini.

Jukwa la Madini Tanzania kimehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya STAMICO Meja General (Mstaafu) Michael Isamuyo, Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse, Katibu Mtendaji Chemba ya Migodi Benjamini Mchwampaka na wawakilishi kampuni ya Mamba, GGM, Jitegemee Holding, ESAP Mining Service Ltd, Yaya Resources na wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini.
Previous Post Next Post