TFS YAAZIMISHA SIKU YA MAPINDUZI KWA KUPANDA MIKOKO JIJINI DAR ES SALAAM


Na Mwandishi Wetu 

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imesema kuwa itabomoa majengo yote yaliyojengwa kwenye Hifadhi za Mikoko iliyopo pembezoni mwa fukwe za bahari siku yoyote kuanzia sasa.

Akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Godwin Gondwe,Katibu Tawala wa halmashauri hiyo Stella Msoffe alisema hayo wakati akiongoza zoezi la upandaji mikoko 350 ilililoratibiwa na Wakala wa Misitu Tanzania ( TFS), ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Miaka 59 ya Mapinduzi Zanzibar.


Pamoja na ubomoaji huo, Msoffe alionya wote wanaojihusisha na uharibifu wa mazingira ya fukwe za bahari na mikoko hiyo kuwa serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria.

" ninatoa rai kwa wananchi wa Kunduchi na wengine walio karibu na mwambao kutojihusisha na uharibifu wa mazingira unaoathiri mikoko na maendeleo ya mazao ya bahari.

" Serikali inahakikisha mazingira yote ya bahari yanalindwa," alisema.


Naye Kaimu Kamanda wa TFS, Kanda ya Mashariki inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam, Pwani na Morogoro, Mathew Ntilicha aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi – TFS Prof. Dos Santos Silayo alisema wameadhimisha sherehe hizo za mapinduzi kwa kupanda miche hiyo.

Alisema kama nchi inapitia mabadiliko ya tabianchi hivyo mikoko ni misitu muhimu katika kukabiliana na hali hiyo pia ina uwezo wa kunyonya hewa chafu mara 10 ya misitu ya asili. 


Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa Hifadhi za Mikoko, Mhifadhi Mkuu wa TFS, Frank Sima alisema nchini Tanzania kuna Wilaya 14 zenye mikoko katika mikoa ya Tanga, Pwani, Dar es Salaam, Lindi na Mtwara.

Alisema upandaji huo wa mikoko ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan za uhifadhi wa mazingira.


Mhifadhi Mkuu Wilaya ya Kinondoni, Dotto Ndumbikwa alisema wamepanda mikoko hiyo katika eneo la Kunduchi Mtongani baada ya kuthiriwa na mtu aliyekuwa na tatizo la akili ambaye alikuwa akikata kwa kile alichokuwa akidai kuwa eneo hilo ni mali yake.


Previous Post Next Post