NHC WAINGIA MAKUBALIANO NA MWEKEZAJI KING JADA KWA AJILI YA UPANGISHWAJI KWENYE MRADI WA MOROCCO SQUARE


Na Mwandishi Wetu

Shirika la nyumba la Taifa (NHC) na wameingia makubaliano na mwekezaji KingJada Hotel and Apartments kwaajili ya upangishwaji wa hoteli kwenye mradi Morocco square.

Sehemu hiyo ni muhimu sana kwa sababu ndiyo inayokamilisha dhana nzima ya mradi huo ya kuishi, kufanya kazi, kununua bidhaa na kupata mapumziko mahala pamoja.


Aidha uwekezaji huo unachagizwa na jitihada nzuri zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuongeza wawekezaji nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa NHC, Nehemia Mchechu amesema Kusainiwa kwa mkataba wa upangaji na uendeshaji wa hoteli hiyo ni ishara ya kuwa katika hatua za mwisho za umaliziaji wa ujenzi na hatua za mwanzo za ufunguzi wa mradi.


Aidha amesema Utiaji saini wa mkataba huu wa upangaji wa hotel ya Mradi wa Morocco Square kati ya NHC na KingJada Hotels & Apartments Ltd ni ishara ya uthubutu na imani ya sekta binafsi kwa Shirika na nchi kwa ujumla.

"Hatua hii inatoa ishara kubwa na muhimu sana katika sekta ya miliki kwa kukamilisha mojawapo ya miradi mikubwa sana ya ujenzi Nchini Tanzania."

Pia amesema Utiaji saini huo unawafanya wafanye kazi kwa pamoja kwa karibu zaidi ili kufikia lengo letu la kuwezesha maendeleo ya sekta ya nyumba nchini Tanzania.


"Hii inatupa fursa ya kutambua michango ya taasisi za fedha kwa maendeleo ya Taifa kwa kuwa sekta ya nyumba ina athari mtambuka katika sekta zote za uchumi."

Mbali na hayo Mchechu aliwashukuru wadau wa mabenki kwa jinsi walivyowaunga mkono na imani kubwa walioijenga kwa menejimenti ya NHC na Bodi ya Wakurugenzi ambapo alizihakikishia taasisi za fedha kwamba wameazimia kuiendeleza miradi kama hiyo kwa kutumia fedha za ndani na mikopo.


Pia Mchechu aliwahakikishia wateja wake kuendelea kupata mikopo ya ununuzi wa nyumba kutoka kwa mabenki haya.  

Kadhalika Mchechu alimhakikishia mwekezaji huyo kuwa watampa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutimiza malengo yake na yao waliyojiwekea .

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mawasiliano wa Kingjada Hotels and Apartments LTD, Risasi Mwaulanga amesema wanayo imani kubwa kwamba shirika litafika mbali kimalengo na kimkakati lakini pia wao kama wabia wao kibiashara kufikia malengo yao ya kibiashara.


Pia amesema wanayo imani kubwa na uendeshaji lakini pia mipango ya maendeleo katika suala zima la uwekezaji kwa juhudi za makusudi zinazofanywa na serikali ya awamu ya sita kupitia mamlaka zote kisekta chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Previous Post Next Post