BALILE: 2023 NI MWAKA WA MABADILIKO KWENYE SEKTA YA HABARI NCHINI


Na Humphrey Msechu

Mwaka 2023 ni mwaka wa mabadiliko makubwa kwenye sekta ya habari kufuatia ahadi iliyoahiwa na serikali juu ya kutekeleza kwa vitendo mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania ( TEF ), Deodatus Balile alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Serikali kutekeleza kwa vitendo kile ilichokiahidi kupitia Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari nchini Mhe. Nape Nnauye.

“Mheshimiwa Nape atakumbukwa katika hili, lakini nguvu kubwa kaipata kutokana na mheshimiwa rais kwa positive na jambo hili. Ni matarajio yetu kwamba, mwaka huu wa 2023 utaleta mageuzi katika tasnia ya habari. 

“Sisi huku kwenye mikutano ya wadau tumeshamaliza ambapo kikao cha mwisho tulifanya Novemba 21, 2022 na baadaye tukaongeza na Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 lililofanyika Desemba 18, 2022. Hivyo kilichobaki ni Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 kuwasilishwa bungeni baadaye mwezi huu,” alisema Balile.

Alisema, wadau wa habari wanaamini kuwa mawazo yao waliyokubaliana na serikali katika maeneo yote, ndiyo yatakayokuwemo katika mswaada huo.

Mwenyekiti huyo wa TEF alisema, matarajio ya wadau wa habari ni kuona mswada huo wa mabadiliko ya sheria ukisomwa bungeni Januari mwaka huu.

“Kwanza kabisa utapitia kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kisha utajadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu na baada ya hapo utajadiliwa na Kamati ya Baraza la Mawaziri.

“Ukitoka hapo utajadiliwa na Baraza la Mawaziri, tunarajia itakuwa kati ya Januari 13 na 14, matazamio yetu ni kwamba utasomwa bungeni kwa mara ya kwanza Januari 31, mwaka huu kisha tutakutana na wadau kuzungumza na wabunge baadae utasomwa kwa mara ya pili na utajadiliwa,” amesema Balile.

Balile amesema kwamba kupitia kauli ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye, aliyotoa siku ya Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022 mswada huo utawasilishwa bungeni katika bunge linalokuja.

“Kwa kauli ile ya Mheshimiwa Waziri tunaimani kuwa mswaada huo utaingia katika bunge hili la Januari na maisha mengine yaendelee,”amesema Balile.

Akizungumzia kuhusu mabadiliko ya Sera na Sheria nyingine katika sekta ya habari amesema kuwa hizo wataziona mbele ya safari.
Desemba 18, 2022 akizunumza katika Kongamano la Maendeleo ya Sekta ya Habari 2022, Waziri Nape alisema kuwa Serikali inampango wakurekebisha sekta ya habari kupitia mfumo wa kisheria, ikiwa ni pamoja na kuunganisha Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 na Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta ya mwaka 2010.

Waziri Nape alisema hatua hiyo inatarajiwa kuleta uratibu madhubuti wa sekta hiyo na umoja kati ya wahusika katika magazeti, mitandao ya elektroniki na kijamii kwa kuwa zote ziko chini yake.

“Pamoja na kupitia upya sera ya nchi ya vyombo vya habari, serikali inapanga kuunganisha sheria zinazohusu masuala ya vyombo vya habari na utangazaji, kwa kuwa zote mbili sasa ziko chini ya wizara moja.
“Ninathibitisha kuwa serikali itatuma bungeni kwa ajili ya kupitia marekebisho ya vifungu vya Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ya mwaka 2016 Januari mwakani(mwaka huu),” alisema Waziri Nape.
Previous Post Next Post