UZINDUZI WA SERA YA UBIA YA NHC KUFUNGUA FURSA YA UWEKEZAJI

Meneja Habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Bw, Muungano Saguya (kushoto) akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Novemba 11, 2022 Jijini Dar es Salaam, kuhusu uzinduzi wa Sera ya Ubia ya Shirika hilo utakaofanyika Novemba 16,2022 Jijini Dar es Salaam.


Na Humphrey Msechu

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) linatarajia kukutana na wadau takribani 1000 kutoka katika Taasisi mbalimbali za Serikali na Binafsi, vyama na Bodi za Kitaaluma, pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi ambao wamethibitisha kushiriki kwenye uzinduzi wa Sera ya ubia ya Shirika hilo utakaofanyika Novemba 16,2022 Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 11,2022 katika Ofisi za Shirika hilo Jijini Dar es Salaam, Meneja Habari na Uhusiano wa NHC Bw, Muungano Saguya amesema kuwa Shirika hilo linakwenda kuzindua sera hiyo iliyoboreshwa na kwamba maboresho hayo yamezingatia maslahi ya Wabia, Shirika la Nyumba la Taifa, na Taifa kwa ujumla.

Amesema kuwa kuzinduliwa kwa sera ya ubia kunaenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na kwamba Shirika linaunga maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuvutia wawekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini yakuleta na kujenga uchumi wa Taifa letu.

“Baada ya kuanza kuutangazia Umma juu ya jambo hilo jema la uzinduzi wa Sera hiyo, kumekuwa na muitikio mkubwa wa makampuni binafsi ya ndani na nje ya nchi wa kushiriki uzinduzi huo”

Aidha Saguya amesema kuwa katika uzinduzi huo pia zaidi ya Balozi 20 na Taasisi za Kimataifa 10 zitashiriki. Wengine ni kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Wenyeviti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), na kamati ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma (PIC), Mawaziri, Mhimili wa Mahakama, Taasisi za Fedha na wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi wamekubali kushiriki.

“Kumekuwa na utayari mkubwa wa Makampuni na taasisi binafsi za nje na ndani ya nchi kutaka kuwekeza katika ujenzi wa majengo makubwa kwenye viwanja vya NHC. kutokana na hali hiyo, Shirika limeona ni vema kuchambua na kuainisha zaidi maeneo ya kutosha ya kukidhi shauku hiyo ya kujenga nchi yetu. hapo hawali tulitenga maeneo 60 tu yenye viwanja/majengo yanayohitaji kuendelezwa. Kwa msukumo uliopo sasa tumeamua kuongeza maeneo zaidi ili yaendelezwe” ameongeza Saguya 

Akifafanua zaidi amesema kuwa Shirika hilo linatayarisha vitabu viwili vitakavyoelezea sera ya ubia na maeneo ya uwekezaji ya NHC yaliyopo, yakielezea taarifa zote muhimu kwa kina.

Sera hiyo ya Ubia ambayo NHC wamewaalika wawekezaji kushiriki ilianzishwa na Shirika hilo tangu mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika. Maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2022 ili kuondoa changamoto zilizojitokeza hapo awali

Tangu kuanza kwa utaratibu huu, jumla ya miradi 111 ilitekelezwa ikiwa na thamani ya TZS Bilioni 300. katika miradi hiyo, miradi 81 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 240 imekamilika na kuanza kutumika, na miradi 30 yenye thamani ya TZS Bilioni 60 imeendelea kukamilishwa.
Previous Post Next Post