Na Humphrey Msechu
Balozi mwakilishi wa umoja wa nchi za Ulaya nchini Tanzania anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kongamano la 13 la kimataifa ambalo linaandaliwa kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) lenye lengo la kuendeleza malengo ya umoja wa Mataifa juu ya matumizi ya uhandisi na teknolojia katika kukabiliana na athari za tabia ya nchi.
Hayo aliyasema Mjumbe wa baraza la taasisi ya wahandisi Tanzania, Mhandisi Makulilo Kassera wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kongamano hilo linalotazamiwa kufanyika tarehe 1 -3 Disemba 2022 katika ukumbi wa kimataifa Arusha (AICC).
Mhandisi Kassera alisema zaidi ya wahandisi na mafundi 1000 kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika kongamano hilo lakini pia baadhi watashiriki kwa njia ya mtandao.
Pia Mhandisi Kassera alisema kupitia kongamano hilo, wanatarajia athari zote za tabia nchi zitatatuliwa na jamii ya kihandisi Tanzanzia.
"Baada ya kongamano hili ni matarajio ya Taasisi kwamba jamii ya kihandisi Tanzanzia itakuwa mshiriki wa utatuzi wa athari za Tabianchi, sote tunazo taarifa za mikutano mbalimbali za kitaifa na kimataifa juu ya athari za Tabianchi na mipango mikakati ambayo imeashimiwa na mikutano hiyo"
Kadhalika, Mhandisi Kassera aliwakaribisha wadau wote wa sekta ya uhandisi kushiriki kwenye kongamano hilo lakini pia aliwataka wahandisi na mafundi ambao bado hawajajiunga na taasisi waweze kujiunga.
Mbali na hayo Mhandisi Kassera alimpongeza Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa msimamo wake akihimiza wasaidizi wake hususani waziri anayehusika na mazingira kuzingatia mipango ya kuinusuru nchi kutokana na athari za tabia nchi.
Kuhusu Taasisi hii ya wahandisi Tanzania, ni Taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa kwa madhumuni ya kukuza fani ya uhandisi na Sayansi Tanzania na nje ambayo mpaka sasa inakisiwa kuwa na jumla ya wanachama 4,644 ambapo katika idadi hiyo asimilia 30 ni wahandisi waandishi, asilimia 50 ni wahandisi wahitimu , Fellow asilimia 2, mafundi asilimia 18 na jumla ya wanafunzi ni takribani 920 kutoka vyuo mbalimbali nchini.