Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara NHC Bw. William Genya, (wa kwanza kulia) akizungumza na Waandishi wa Habari (hawapo pichani). Katikati ni Meneja Habari na Uhusiano NHC Bw. Muungano Saguya na kushoto mwisho ni Afisa Habari NHC Bi. Domina Rwemanyila.
Meneja Habari na Uhusiano NHC Bw. Muungano Saguya akifafanua jambo kwa Wanahabari (hawapo picha) katika mkutano huo
Na Mwandishi Wetu,
SHIRIKA la Nyumba (NHC),linatarajia kuanza kubomoa nyumba zilizochakaa
katika maeneo ya Kariakoo na Posta jijini Dar es Salaam pamoja na kuendeleza viwanja 40 vilivyopo mkoani humo kikiwemo cha eneo iliyokuwa klabu ya Bilicanas.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uendelezaji Biashara wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), William Genya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na uzinduzi wa sera ya ubia ya shirikia la Nyumba la Taifa.
Amesema kuwa hatua hiyo inatokana na kuwepo kwa upungufu ya nyumba za wapangaji hivyo NHC katika mwendelezo wa utekelezaji wa miradi ya Shirika la Nyumba la Taifa chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu Bw.Nehemiah Kyando Mchechu itaingia ubia na sekta binafsi ili kufanikisha ujenzi wa nyumba hizo.
“Kuna upungufu mkubwa wa uhitaji wa nyumba za wapangaji hivyo NHC itaingia ubia na sekta binafsi na kuboa nyumba ambazo zinaonekana kuchoka ama kuzeeka katika maeneo ya Kariakoo mtaa wa Tandamti, Msimbazi,Uhuru,Nyamwezi na pia kuendeleza viwanja vya wazi kwa kujenga nyumba za miradi.
“Kuna viwanja 60 vinavyotakiwa kujengwa nyumba za wapangaji kati ya hivyo 40 vipo Mkoa wa Dar es Salaam na 20 vipo mikoani amnavyo navyo vitajengwa nyumba za wapangaji.
“Pia kuna eneo la wazi ambalo linatumika kwa Parking Posta nalo litatumika kwa ujenzi wa nyumba za wapangaji na viwanja vingine vipo mkoa ya Mwanza, Arusha lakini kabla ya kuanza miradi hiyo titazungumza na wahusika ili kuweka mambo sawa,’ amesema.
Amesema kuwa NHC ina vipaumbele 11 ambavyo vinaenda kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha 2022/23 hivyo hatua iliyofikiwa wa vipeumbele hivyo itatangazwa Oktoba 21, mwaka huu kwenye uzinduzi ya ubia ya shirikia la Nyumba la Taifa inayotarajia kufanyika Dar es Salaam.
“Uzinduzi wa sera hii iliyoboreshwa ili kuwa na maslahi mapana kwa Shirika, wawekezaji na Taifa kwa ujumla, unalenga kuwapatia fursa wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini.
“Uzinduzi wa Sera ya Ubia unaenda kufungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba na kwa hakika tunaunga mkono maono na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binafsi ambayo ni injini ya kuleta maendeleo ili iwekeze mitaji yao kujenga uchumi wa Taifa letu,” amesema.
Meneja wa Habari na Mawasiliano NHC, Muungano Saguya amesema kuwa kauli mbiu ya uzinduzi wa sera hii ni “Tunajenga Taifa letu kwa Ubia na Sekta Binafsi”. Kauli mbiu hii inahimiza ushiriki wa sekta binafsi katika kuendeleza maeneo yaliyopo katikati ya miji ambayo yana thamani kubwa kuliko majengo majengo yaliyopo sasa, ili kukuza mapato ya Shirika.
Saguya amesema kuwa sera ya ubia ambayo tunawaalika Watanzania kushiriki ilianzishwa na Shirika tangu mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika.
“Maboresho ya mwisho yalifanyika mwaka 2022 na yamezingatia kuvutia uwekezaji kwa kuwa yana maslahi kwa Shirika na mwekezaji. Tangu kuanza kwa utaratibu huu, jumla ya miradi 111 ilitekelezwa ikiwa na thamani ya sh Bilioni 300. Katika miradi hiyo, miradi 81 yenye thamani ya shilingi bilioni 240 imekamilika na kuanza kutumika na miradi 30 yenye thamani ya sh.Bilioni 60 inaendelea kukamilishwa,’ amesema.
Amesema kuwa miradi hii imechangia upatikanaji wa ajira, kuboresha mandhari ya miji yetu, kuongeza mapato ya Shirika, kuongeza wigo wa kodi za serikali, kuongeza maeneo kwa ajili ya biashara na makazi na kuipanga miji yetu.
“Katika uzinduzi huu mkubwa tunakusudia kuwa na washiriki takribani 600 kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na binafsi; vyama na bodi za kitaaluma pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi ambao wamealikwa. Aidha, mabalozi wa nchi zenye wawekezaji wakubwa wamealikwa na wawakilishi wa Kamati za Bunge zinazogusa shughuli za Shirika wamealikwa,’ amesema.