MAKUNGA: WAANDISHI WA HABARI NI WATU MUHIMU KATIKA KUSIMAMIA NA KUTETEA DEMOKRASIA NCHINI


Na Humphrey Msechu 

MWENYEKITI mstaafu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania TEF Theophil Makunga amesema Waandishi wa habari ni watu muhimu katika kutetea na kusimamia Demokrasia katika nchi endapo watafanya kazi yao kwa uhuru na demokrasia inakua huru zaidi .

Makunga ameyasema hayo Leo Alhamisi Oktoba 20, 2022 wakati wa semina ya kuwajengea uwezo Waandishi wa habari kuandika habari zinazohusu kampeni ya mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari ya mwaka 2016 ikiwa ni sehemu ya kufungua mradi wa kufanya uchechemuzi kwenye mabadiliko ya sheria hiyo.

Semina hiyo ni muendelezo wa vikao kati ya jukwaa la Wahariri Tanzania TEF na wadau wa habari katika mchakato wa mapendekezo ya wadau kutaka mabadiliko Kwenye baadhi ya vifungu kandamizi kwenye sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kikao hicho Makunga ameishukuru Serikali kwa kukubali kupokea mapendekezo ya wadau wa habari kuhusu mchakato wa marekebisho ya baadhi ya vifungu vya sheria hiyo ambavyo vimekua vikilalamikiwa na wadau kwa kubana uhuru wa vyombo vya habari.

Amesema unapompa mwandishi nafasi ya kufanya kazi yake kwa uhuru unasaidia kusukuma maendeleo katika nchi.

" Naamini kwamba tunapoelekea kuna mwanga unaonekana mbele wa kuwafanya waandishi wa habari waweze kufanya kazi kwa uhuru ili kuleta maendeleo ya nchi "

Amesema watawala wengi duniani wanapenda vyombo vya habari viandike habari za kuwasifia hivyo kunapokua na vyombo vya habari vinavyokosoa na kuweka wazi katika jamii wanasiasa wengi huwa hawapendi.

" Unapompa uhuru mwandishi wa habari unamsaidia kuchuja mambo ya kuandika na ambayo hayafai kuandikwa kwa uhuru wake lakini ukiweka sheria ambazo zinazomzuia hawezi akafanya kazi vizuri"
Previous Post Next Post