BYABATO AWATAKA WANANCHI MBARALI KUTOINGIZA MIFUGO KWENYE VYANZO VYA MAJI

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akizungumza na wananchi wa Kata ya Ubaruku wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta walipofanya ziara kwenye eneo la Mto Ruaha Mkuu mkoani Mbeya. 

Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakiongozwa na Mwenyekiti wao Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula (wa tatu kulia) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili Mbarali mkoani Mbeya kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya Matumizi ya ardhi. Katikati ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato.

Mawaziri wa Wizara za Kisekta wakiongozwa na Mwenyekiti wao Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula, wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Juma Homera walipokwenda kutazama na kujionea hali halisi ya upungufu wa maji katika mto Ruaha Mkuu.


Na Mwandishi Wetu 

Naibu waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amewataka wananchi wa Kata ya Ubaruku Mbarali mkoani Mbeya kutoingiza mifugo kwenye vyanzo vya maji badala yake wavitunze ili visaidie katika upatikanaji wa nishati ya umeme nchini.
 
Byabato aliyasema hayo tarehe 25 Oktoba, 2022 katika mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo la Ubaruku, Mbarali wakati Kamati ya Mawaziri Nane wa Wizara za Kisekta walipofanya ziara kwenye eneo la Mto Ruaha Mkuu ambapo Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imetangaza kwamba vijiji vitano na vitongoji 41 na sehemu ndogo ya kitongoji cha Magwalisi ambacho kipo kwenye Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa wilayani Mbarali wananchi wanatakiwa kuhamishwa ili kupisha hifadhi.
 
Lengo la uamuzi huo wa Serikali ni kutunza na kulinda ardhi oevu na vyanzo vya kupokea na kutunza maji yanayotiririka kutoka mito mbalimbali.
 
Byabato alisema kuwa, Mto Ruaha ni moja ya mito inayotegemewa kupeleka maji katika bwawa la Mtera na Bwawa la Julius Nyerere hivyo ni vyema ukatunzwa na kuhifadhiwa kwa maslahi mapana ya nchi.
 
"Tunakubaliana kuwa shughuli zote zinatuhusu sisi wenyewe na sisi Wizara ya Nishati tunayategemea maji hayohayo kuweza kuzalisha umeme, na umeme ukishazalishwa tunautumia kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kwenye viwanda vyetu vinavyochakata mazao mbalimbali hivyo, wanambarali tutunze vyanzo vyetu vya maji”. Alisema Byabato
Previous Post Next Post