WALIOPATA UFAULU WA JUU MASOMO YA SAYANSI WAITWA


Na Humphrey Msechu

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amefungua rasmi dirisha la ufadhili wa masomo ya elimu ya juu (Samia Scholarship) ambapo wanafunzi waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya sayansi kwenye mitihani ya kidato cha sita, wataanza kuomba kesho.

Ufadhili huo utahusisha ada ya mafunzo, posho ya chakula na malazi, posho ya vitabu na viandika, mahitaji maalum ya vitivo, vifaa saidizi kwa wenye mahitaji maalum na bima ya afya.

Profesa Mkenda ametangaza kufunguliwa kwa dirisha hilo leo Jumanne Septemba 27, 2022 katika mkutano wa wadau wa elimu wa kujadili rasimu ya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na mitaala ya elimu.

Amesema majina ya wanafunzi hao yanapatikana kuanzia leo katika tovuti ya Wizara www.moe.go.tz na ya Bodi ya Mikopo ya wanafunzi wa Elimu ya Juu www.heslb.go.tz. 

Aidha wanafunzi hao wataanza kuomba ufadhili huo kuanzia  kesho Septemba 28, 2022  kupitia tovuti ya Bodi ya Mikopo ya Mikopo https://olas.heslb.go.tz kwa siku 14.

Akitoa tangazo hilo leo Septemba 27, 2022 jijini Dodoma Waziri Mkenda amesema wanafunzi hao watafadhiliwa kwa asilimia mia moja kwa kipindi cha miaka mitatu hadi mitano kulingana na programu husika walizodahiliwa.

Amefafanunua kwamba wanafunzi hao ni wa Tahasusi za sayansi ambazo PCB, PCM, PGM, CBG, CBA, PMC na CBN.
 
"SAMIA SCHOLARSHIP itagharamia kwa asilimia mia moja masomo ya Chuo Kikuu kwa wanafunzi ambao wamepata udahili katika fani za Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba katika Vyuo Vikuu vya hapa nchini vinavyotambulika na Serikali ," amesema Waziri Mkenda

Prof. Mkenda amesema ufadhili huo utazingatia viwango na miongozo ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya juu kwa kugharamia ada ya mafunzo, Posho ya chakula na malazi, vitabu na viandikwa, mahitaji maalum ya vitivo, mafunzo kwa vitendo, utafiti, vifaa saidizi kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum na bima ya Afya.

Waziri Mkenda ametaja masharti saba ya ufadhili huo ikiwemo kiwango cha ufaulu wa mnufaika kisiwe chini ya GPA 3.8 katika mwaka wa masomo na chini ya hapo ufadhili utasitishwa.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Ali Abdulgullam Hussein amepongeza hatua ya Serikali kutoa ufadhili huo  ambapo kwa upande wa Zanzibar ufadhili wa aina hiyo pia umetolewa kwa wanafunzi 30 hivyo kuongeza fursa kwa watoto wa kitanzania kupata elimu ya juu.  

Previous Post Next Post