Tanzania Yaanza Kufikia Mabadiliko Endelevu ya Kidijitali



Na Innocent Mungy, Bucharest
 
Tanzania inatekeleza mfumo wa Taifa wa Uchumi wa Kidijitali, ambao utahakikisha sekta zote za uchumi zinatumia TEHAMA huku ikiwezesha mabadiliko ya kidijitali yanayojenga jamii jumuishi ya kidijitali kwa ajili ya maendeleo endelevu.
 
Hayo yalisemwa na Mheshimiwa Nape Nnauye (Mbunge), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wakati akiwasilisha Tamko la Kisera la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano Duniani (ITU PP 2022) unaofanyika hapa Bucharest, Romania.
 

 
Mheshimiwa Nape alisema Tanzania ina Sera ya Taifa ya TEHAMA, ambayo imesababisha ongezeko kubwa la matumizi ya TEHAMA katika sekta mbalimbali za uchumi. Tanzania pia imewezesha ujumuishaji wa kifedha ambao umehusisha idadi ya watu wa Tanzania ambao hawakuwa wanapata huduma za kibenki hasa jamii ya vijijini. Alihusisha mafanikio hayo na ushiriki wa Sekta Binafsi.
 
"Tangu tuanzishe Mfumo wa Leseni uliounganishwa mwaka 2005 ili kuinua TEHAMA katika jitihada zetu za kuinua ustawi wa kijamii na kiuchumi wa watu wetu, tumeona mafanikio. Shukrani kwa mikakati ya ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi. Tanzania imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika suala zima la ujumuishaji wa kifedha (Financial Inclusion). Leo hii kuna zaidi ya watumiaji milioni 35.75 wa huduma za fedha kupitia simu ikilinganishwa na watumiaji milioni 23.34 mwaka 2018" alisema Mhe. Nape Nnauye.
 


Serikali ya Tanzania imewekeza maelfu ya kilomita za Mkongo wa Taifa wa TEHAMA (NICTBB). Mheshimiwa Nnauye alisema kuwa mipango ya uunganishaji wa Mkongo wa Mawasiliano kwa nchi jirani na zisizo na bandari ni ahadi ambazo Tanzania imekuwa ikizipa kipaumbele sana. Mkongo wa Taifa unaunganisha nchi zisizo na Bahari kupitia maeneo ya mpakani ya Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia na Malawi. Mkongo huu una urefu wa KM 18,000.
 


"Ili kupata mitandao ya mawasiliano, mifumo ya habari na upatikanaji wake, Tanzania imeanzisha Timu yake ya Taifa ya Kukabiliana na Dharura ya Usalama wa Kompyuta (TZ-CERT) ili kuratibu matukio ya kimtandao katika ngazi ya kitaifa" alieleza Mheshimiwa Nape Nnauye.  
Previous Post Next Post