SERIKALI KUENDELEA NA MCHAKATO WA KUTIZAMA UPYA MITAALA YA ELIMU ILI KUTATUA CHANGAMOTO ZA AJIRA



Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaendelea na mchakato wa kutazama upya Sera, Sheria na Mitaala ya Elimu ili kutatua changamoto za ajira kwa wahitimu wa vyuo vya elimu ya juu.

Kipanga amebainisha hilo leo jijini Dar es Salaam wakati akimuwakilisha Waziri Elimu, Prof. Adolf Mkenda katika mahafali ya tatu ya wahitimu wa elimu ya juu nje ya nchi chini ya uratibu wa Taasisi ya Global Education link ambapo amesema serikali pia itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ili kutimiza adhma ya Rais Samia Suluhu Hassan la kutatua majawabu ya changamoto mbalimbali katika sekta ya elimu nchini.



Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Ali Abdulgulam Hussein amewataka wahitimu kuacha kutegemea ajira serikalini na kuanza kuwa na fikra za kujiajiri kwakuwa serikali haina uwezo wakuajiri kila mtu kutokana na idadi kubwa ya wahitaji kila siku.


Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Education Link, Abdulmalik Mollel ameitaka serikali kuangalia namna ya kuwawezesha vijana wanaosoma nje ya nchi kwa kuwapatia mikopo kama ambavyo wanapataiwa wanafunzi ndani ya nchi.


Jumla ya Wahitimu 400 wa Elimu ya Juu nje ya Nchi wamefanyiwa mahafali hiyo ambapo takribani asilimia 50 ya wahitimu hao wanatokea upande wa Afya, waliobobea katika masuala ya Saratani na Upasuaji ikiwemo wa Moyo.
Previous Post Next Post