NEVILLE Meena, Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), amesema Watanzania wamerejea kufuatilia habari kutoka katika Magazeti, Radio na Televisheni.
Na kwamba, hali hii ilikuwa imepotea katika miaka michache iliyopita kutokana na tasnia ya habari kupita katika mazingira magumu.
Meena ametoa kauli hiyo wakati akizungumza katika Kipindi cha Hali Halisi kinachorushwa na Kituo cha Radio Upendo Jijini Dar es Salaam.
Amesema, Watanzania walikuwa hawakimbilii magazeti, Televisheni wala Radio kupata habari, waliamini hakuna kile walichokihitaji. Walikuwa wakiamka, moja kwa moja wanamtafuta Mange Kimambi na Kigogo kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii, waliamini kule ndio watapata taarifa halisi. Wengi waliacha kabisa kusoma magazeti, kusikiliza radio na kuangalia habari katika Televisheni.
Ni kauli ya Neville Meena, Mjume wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), akizungumza katika Kipindi cha Hali Halisi kinachorushwa na Kituo cha Radio Upendo leo tarehe 11 Agosti 2022, Jijini Dar es Salaam.
Amesema, hiyo ni moja ya athari iliyojitokeza nchini kutokana na kutokuwepo kwa uhuru wa vyombo vya habari.
“Watu walikuwa wakitafuta habari na hawapati zile walizozitaka. Kuna watu walisema, wameacha kusoma magazeti, kuangalia Televisheni na pia kusikiliza Radio, waligeukia kwenye mitandao ya kijamii.
"Wakiamka walikuwa hawakimbilii gazeti, ni wakati ambao tuliambiwa kuna uhuru wa habari kwa sababu kuna usajili wa televisheni, majarida na magazeti karibu 500,” amesema.
Meena ambaye pia ni Katibu Mstaafu wa TEF amesema, mazingira hayo ndiyo yaliyounganisha wadau wa habari nchini katika kutafuta muafaka.
Na kwamba, mambo mengi yaliyochangia kutia hofu wanahabari ni pamoja na kuwepo kwa sheria zenye mtego, ikiwemo utaratibu wa kuomba leseni ya kuendesha gazeti kila mwaka.
“Ikiwa umesajili kampuni na ukapewa leseni, kisha ukasajili gazeti, kuna haja gani kampuni hiyo ikawa kila mwaka inaomba lesini kwa ajili ya kuendesha gazeti?
“Haya, huyo Mkurugenzi wa Habari Maelezo anayo hiyari ya kukupa leseni ama kutokupa. Tumeona magazeti kama MwanaHalisi hata baada ya kushinda kesi na pia kumaliza kifungo, yalinyimwa leseni. Tukasema hili sio jambo jema, tunapendekeza usajili uwe mara moja na kusiwepo mambo ya leseni,” amesema Meena.
Amesema, wanahabari wangependa kuona wananchi wanafanya rejea katika vyombo vya habari kupata ukweli. Ameeelza kwamba, hatua ya sheria kuelekeza Mkurugenzi wa Habari Maelezo kuwa mgawa matangazo ya serikali, inazidisha ukakasi.
“Vyombo vya Habari vinajiendesha kwa matangazo na huu ni ushindani wa kibiashara, sasa taasisi zote za serikali kulazimishwa kupeleka matangazo kwa Mkurugenzi wa Habari Maelezo ili ayagawe, sio sawasawa.
“Hii maana yake, kama chombo chako cha habari kimetafsiriwa kuandika kile ambacho serikali haikitaki, basi huwezi kupata matangazo. Huku ni kuua vyombo vya habari kiuchumi. Jambo hili liachwe kwenye ushindani wa kibiashara pekee,” amesema.
Akizungumzia baadhi ya vipengele vilivyobeba tasnia ya habari katika Sheria ya Habari ya Mwaka 2016, amesema ni pamoja na wanahabari kutambulika kama taaluma rasmi.
“Sio kila kilichokuwemo kwenye sheria iliyopo sasa hakifai, Hapana. Sheria hii ndio kwa mara ya kwanza imetambua habari kama taaluma na mwanahabari anafanya kazi kwa mujibu wa sheria.