Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Happy Msimbe, akizungumza katika kikao kilichowakutanisha Wataalam wa Sheria kutoka Taasisi za Serikali kwa lengo la kujadili uwezekano wa Makosa ya Ulawiti na Ubakaji kutokuwa na dhamana ili kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, jijini Dodoma.
Afisa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Ignas Mwinuka akiwasilisha maoni yake katika kikao kilichowakutanisha Wataalam wa Sheria kutoka Taasisi za Serikali kwa lengo la kujadili uwezekano wa Makosa ya Ulawiti na Ubakaji kutokuwa na dhamana ili kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, jijini Dodoma.
Baadhi ya Wataalam na wadau wa masuala ya Sheria kutoka Wizara, Taasisi za Serikali wakijadiliana katika Makundi kuhusu uwezekano wa Makosa ya Ulawiti na Ubakaji kutokuwa na dhamana ili kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma.
Na WMJJWM Dodoma
Serikali imesema imeanza kukutana na wadau mbalimbali wa masuala ya Sheria kuona uwezekano wa kuondoa dhamana ya makosa ya Ubakaji na Ulawiti ikiwa ni jitihada za kupunguza malalamiko ndani ya jamii na kulinda kundi la Watoto na Wanawake kutokana na vitendo vya ukatili dhidi yao.
Hayo yamebainika jijini Dodoma Juni 20, 2022 kwenye kikao kilichowakutanisha Wataalam na wadau wa masuala ya Sheria kutoka Wizara, Taasisi za Serikali kwa lengo la kutoa mapendekezo ya Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Happy Msimbe alisema nia ya kukutana na wataalam hao ni kupata maoni yatayosaidia kujenga hoja ya kufanya makosa ya Ulawiti na Ubakaji kutokuwa na dhamana ili kusaidia kupungua kwa makosa hayo na kuwalinda Watoto na Wanawake na vitendo vya ukatili.
Ameongeza kuwa sambamba na hayo kikao hicho kimelenga kuangalia na kupitia Sheria nyingine ambazo zinamgusa mtoto ili ziweze kuendana na hali halisi iliyopo katika jamii ili kuwasaidia Watoto wanafanyiwa Vitendo vya ukatili katika jamii.
"Sisi timu ya Wataalam tumekutana hapa kwa kusudi la kujadiliana na kuona uwezekano wa kuondoa dhamana katika makosa ya Ulawiti na Ubakaji ili iweze kusaidia" alisema Bi. Happy
Kwa upande wake Afisa kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Ignas Mwinuka alisema kuwa nia ya kukusudiaa kutokuwa na dhamana katika makosa ya Ulawiti na Ubakaji wameangalia pia katika Sheria mbalimbali zikiwemo Sheria za Zanzibar ambazo zimeweka kosa la Ulawiti kutokuwa na dhamana ili kusaidia kuwalinda Watoto na Wanawake dhidi ya vitendo hivyo.
Ameongeza kuwa katika tafiti ndogo waliyofanya inaonesha kuwa makosa hayo ya Ulawiti na Ubakaji baadhi ya Watuhumiwa wakiwa nje kwa dhamana wamekuwa wanakimbia na kutoweka na wengine kuharibu ushahidi au kumalizana na wazazi au ndugu wa muathirika wa vitendo hivyo.
"Tumeangalia baadhi ya makosa na kuwa hasa kosa la Ulawiti hata ukilizingumza kwa jamii itakwambia kuwa ni sahihi kukosa dhamana hasa katika kulinda mila na desturi zetu " alisema Mwinuka.
Pia wadau na Wataalam hao wamejadiliana namna bora ya kuhakikisha jamii inapata elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili kwa kutoa taarifa ya vitendo hivyo vinavyotokea ndani ya jamii.
Kikao hicho kimeandaliwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kupitia Kitengo cha Huduma za Sheria.