Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inakwenda kutengeneza studio kila wilaya kwa ajili ya kurekodia kazi za sanaa.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya leo Julai 3, 2022 wakati akifunga tamasha la kwanza la kitaifa la utamaduni katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Aidha amesema wizara yake inakwenda kutekeleza maelekezo ya viongozi wetu ya kuthamini, kuandaa mavazi ya taifa ili kuhakikisha mila na desturi za mtanzania zinaendelezwa.
" Maelekezo ya viongozi wetu ni sheria, amri iwe jua, iwe mvua sisi Wizara, tutawajibika kutekeleza bila kusita wala kuchelewa" amesisita Mhe. Mchengerwa
Pia amesema wizara imejipanga vizuri kuhakikisha Tamasha la kitaifa la pili la Utamaduni litakalofanyika mwakani litakuwa katika kiwango cha kimataifa.
Ameongeza kuwa kumalizika kwa tamasha hili ni mwanzo wa kuanza maandalizi ya matamasha kwenye mikoa na wilaya zote nchini ambapo ametaka maafisa utamaduni kulisimamia hili.
"Ni matarajio yangu kuwa mikoa yote itakaoanza sisi kama wizara tutakuja mara moja. Tunahitaji watanzania wakae katika furaha katika maisha yao" amefafanua Mhe. Mchengerwa
Amewapongeza wakuu wa mikoa kwa kuwezesha vikundi vya Utamaduni kuhudhuria kwenye tamasha.
Amesema bila Utamaduni taifa hili litaendelea kukopa tamaduni za mataifa mengine.
Aidha, amesema kufanikiwa kwa tamasha hili kuonekana ni kutokana na maono ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
Amesisitiza kuwa tamasha hili litakuwa endelevu na litakuwa linafanyika kwa mzunguko kila mkoa.
Pia amesema Wizara imefanikiwa kulitangaza tukio hili kwa kuwa watu zaidi ya milioni 10 wametazama kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari.
Kwa upande mwingine Selikali imeanzisha Mfuko wa Utamaduni kwa lengo la kuwasaidi wasanii nchini ambapo amesema tayari kwa mwaka 2022/2023 umetengewa shilingi bilioni mbili kwa kazi hiyo.
Amewaomba viongozi wa mila na wananchi kwa ujumla kuendelea kukemea vitendo ambavyo ni kinyume cha maadili ya mtanzania.
Pia amewataka wananchi kushiriki kwenye sensa.
Katika tamasha hilo amekadhi zawadi kwa washindi wa ngoma na vyakula ambapo washindi wa ngoma za asili ni mkoa wa
Mwanza ambao umekuwa namba moja,
Lindi ambao umekuwa namba mbili na mkoa wa
Mjini magharibi umekuwa wa tatu.
Kwa upande wa vyakula vya asili mkoa
Kilimanjaro umeongoza ukifuatiwa na mkoa wa
Tanga na mkoa wa
Kagera umeshika nafasi ya tatu.