Mkuu wa Majeshi ya ulinzi Jenerali Jacob John Mkunda amesema Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMA JKT) limeendelea na shughuli za uzalishaji mali kwa faida ili kuipunguzia Serikali gharama ya malezi ya vijana wanaojiunga na Jeshi la kujenga Taifa kupitia kampuni zake tanzu na viwanda mbali mbali.
Mkunda ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika hafla ya maadhimisho ya kutimiza miaka 41 ya SUMA JKT inayofanyika Mkoani Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi wa hafla hiyo ni Waziri wa ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Stergomena Tax.
Ameeleza kuwa pamoja na shirika hilo kuipunguzia serikali gharama za kuendesha Jeshi la kujenga Taifa, lakini shirika limekuwa likichangia pato la Taifa kwa kutoa gawio na kodi kutokana na bidhaa na huduma zinazozalishwa na shirika hilo.