BADO KUNA UKAKASI WA SHERIA YA HABARI KATI YA MWANDISHI NA CHOMBO CHAKE


JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF) limesema kusudio la maboresho ya Sheria za Habari nchini ni kuwaondoa wanahabari na vyombo vyao katika sintofahamu.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Deodatus Balile akizungumza kwenye kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds Televisheni jijini Dar es Salaam ambapo amesema kuwa suala hilo ni miongoni mwa mabadiliko ya sheria za habari yanayopigiwa chapuo.

Amesema, moja ya kitanzi katika Tasnia ya Habari, ni kosa la mwandishi kuelekezwa kuwa kosa la kituo ama taasisi ya habari.

Amesema, kosa la mwanahabari limekuwa likichukuliwa kama kosa la taasisi ya habari na kusababisha madhara makubwa ya kufungwa kituo ama gazeti tofauti na ilivyo kwenye tasnia nyingine nchini.

“Kosa la mwandishi mmoja, unafungia kituo ama gazeti? Kuna watu wengi wanaumia hapo. Yupo dereva ambaye wala hahusiki na habari iliyochapishwa lakini hata mwananchi ambaye hupata habari kwenye chombo anachokipenda, anakuwa ameumizwa,” amesema Balile.

Ametoa mfano wa daktari aliyemfumua nyuzi mgonjwa baada ya kushindwa kulipa Sh 10,000 gharama za matibabu: “Huyu daktari, waziri hakumfukuza kazi, alimpeleka kwenye bodi ya madaktari na wao wakachukua hatua stahili,” amesema Balile.

Amesema, iwapo Bodi ya Ithibati ya Habari itakuwa huru na kujumuisha wadau mbalimbali wa tasnia hiyo, itakuwa na ufanisi mkubwa na kujengea heshima tasnia hiyo.
Previous Post Next Post