HIVI NDIVYO VIFUNGU VYA SHERIA AMBAVYO WADAU WA HABARI WAMEPENDEKEZA ZIFUTWE KUTOKA KWENYE SHERIA YA HABARI YA 2016



Na Humphrey Msechu 

Ikiwa Serikali inaendelea na mchakato wa mabaoresho ya Sheria ya habari, Wadau wa habari Tanzania wameendelea kuwasilisha serikalini mapendekezo mbalimbali ya mabadiliko ya sheria ya habari ya nchini hapa kwa lengo kuondoa baadhi vipengele vya sheria hiyo huku wakishauri baadhi ya vipengele kuondolewa kabisa kutokana na kuwa na matatizo na kuwa kandamizi dhidi ya watoa huduma wa sekta ya habari.

Sheria hii ambayo ilipitishwa rasmi na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Novemba 5 mwaka 2016 na kutiwa saini na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli Novemba 16, 2016 ambapo ilianza kutumika rasmi, wadau wa habari nchini hapa wakiwemo waandishi wa habari, wahariri, wanasheria na wadau wengine wameeleza kuwa bado zipo sheria zinazotoa mianya ya kuminywa uhuru wa vyombo vya habari nchini.

Serikali imetoa mapendekezo juu ya mabadiliko ya sheria ya Huduma za Habari (Media Services Act), 2016 lakini wadau wanapendekeza mabadiliko zaidi kwenye baadhi ya maeneo huku wakibainisha kuwa mapendekezo hayo yameambatana na mifano bora ya sheria zinazoendesha vyombo vya habari na uhuru wahabari kwenye nchi nyingine za Kiafrika. 

Miongoni mwa vifungu ambavyo wadau wamependekeza vifutwe ni pamoja na Kifungu cha 5 (1) amabacho kinatoa mamlaka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kuratibu matangazo yote yanayotoka Serikalini.

Wadau wanasema kuwa changamoto ya kifungu hiki ni kwamba Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo ndio mshauri mkuu wa Serikali kwenye masuala ya habari, uchapishaji na utendaji wa vyombo vya habari. Kumpatia mamlaka ya kuratibu masuala ya matangazo anaweza kuwa na upendeleo na kunyima matangazo kwenye magazeti ambayo yataonekana kuchapisha habari ambazo zina mtazamo tofauti na Serikali, Hivyo basi Hii itafifisha uchipukaji wa mawazo anuwai katika jamii na kukwaza uhuru wa kujieleza.

Wadau wanapendekeza kufutwa kwa kifungu hiki kutatoa nafasi kwa taasisi za Serikali kutoa matangazo yao kwa magazeti wanayoona yanafaa kwao na yenye kufika sehemu kubwa ya nchi. Pia vyombo vya habari binafsi vitanufaika na matangazo hayo. 

Kifungu kingine ambacho wadau wanapendekeza kifutwe ni Kifungu cha 6 na Kanuni ya 8 (3) na 12 ya Sheria za Huduma za Habari amabcho kinaelekeza magazeti na majarida kufanya uhuishaji wa leseni zao kila mwaka.

Changamoto ya kifungu hiki ni kwamba Uhuishaji wa leseni za uchapishaji wa magazeti kila mwaka unaweza kutumiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo kama rungu la kunyima usajili kwa baadhi ya magazeti au majarida ambayo yatakuwa na mtazamo tofauti na Serikali kwenye uchapishaji wa habari zake.Pia Ukataji wa leseni kila mwaka umekuwaF kikwazo kwa mujibu wa sheria hii.

Mfano wa bora wa utekelezaji wa sheria hii katika nchi nyingine ni Ghana ambapo hakuna usajili unaohitajika ili kuendesha biashara ya vyombo vya habari kama inavyoonyeshwa kwenye Ibara ya 162(3) ya Katiba ya Ghana ya mwaka 1992.

Kifungu kingine cha sheria hii amabcho wadau wananpendekeza kifutwe ni Kifungu cha 7 (2) (b)
(iv) cha Sheria ya Huduma za Habari ambacho kinatoa maelekezo kwa vyombo vya habari binafsi kuchapisha habari zenye umuhimu kwa taifa kwa maelekezo ya Serikali. 

Changamoto ya kifungu hiki ni kwamba Kifungu hiki cha Sheria kinaingilia uhuru wa uhariri na hasa kwenye vyombo vya habari vya binafsi, hivyo kikifutwa kitawezesha maamuzi ya kihariri kuzingatia vigezo vya taaluma bila kuathiriwa na maamrisho yasiyo ya kitaaluma. Uhuru wa uhariri (editorial independence) utalindwa.
Previous Post Next Post