Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama akizungumza na wa Muguda wa Kijiji cha Muguda wilayani Kishapu mkoani shinyanga alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR)
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama (kushoto) akikagua ujenzi wa kituo cha kunenepeshea mifugo katika kijiji cha Muguda wilayani Kishapu mkoani shinyanga alipofanya ziara ya kikazi ya kukagua shughuli zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR)
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama (kushoto) akiangalia viatu vilivyotengezwa katika kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi kijiji cha Kiloleli alipofanya ziara ya kikazi wilayani Kishapu mkoani shinyanga kukagua shughuli zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR)
Baadhi ya mashine zilizonunuliwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) zinazotumika katika kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi katika kijiji cha Kiloleli wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Mratibu Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) ngazi ya taifa kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais Dk. James Nyarobi (katikato) akizungumza wakati wa ziara ya kukagua shughuli za mradi huo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama (mwenye Kaunda suti) akisikiliza maelezo kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) alipofanya ziara ya kukagua shughuli za mradi huo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Na Mwandishi Wetu
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama ametoa rai kwa kaya zilitengeneza majiko banifu kusambnaza maarifa hayo kwe kaya zingine ili kusaidia kupunguza ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Ametoa rai hiyo alipofanya ziara ya kukagua shughuli zinazotekelezwa kupitia Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa kutumia Mifumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika vijiji vya Kiloleli, Beledi na Mihama wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Akizungumza kwa nyakati tofauti na wanavikundi vinavyonufaika na mradi huo, Dkt. Mkama aliwataka watumie maarifa waliyopata katika utengenezaji wa majiko hayo rafiki wa mazingira kuwafundisha wengine hatua itakayosaidia kupunguza ukataji miti.
“Niwapongeze kwa kuibeba wilaya katika utengenezaji wa majiko, huu utaalamu wenu muwarithishe wengine na watahamasika mpaka wote watahama kutoka kwenye kukata miti kwa ajili ya kuni hivyo watahamia kwenye majiko,” alisema.
Pia, Naibu katibu mkuu huyo aliwapa tahadhari wananchi hao kuwa ukataji miti unasababisha uharibifu mkubwa wa mazingira na hivyo changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo husababisha upungufu wa mvua.
Aliongeza kuwa miradi hiyo inayotekelezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais itakuwa na msaada mkubwa katika kukabiliana na changamoto za kimazingira hivyo wananchi wanapaswa kuilinda.
Katika hatua nyingine Dkt. Mkama alisema changamoto ya uhaba wa maji katika vijiji hivyo itakuwa historia baada ya kukamilika kwa uchimbaji wa malambo matatu.
Aliwataka wananchi hao kuhakikisha wanayatunza malambo hayo ikiwemo kuyaweka katika hali ya usafi na kuepuka kufanya shughuli zisizotakiwa zikiwemo kufua au kuogelea, pindi uchimbaji wake utakapokamilika.
Wakitoa maoni kuhusu mradi huo Bi. Paulina Selia na Emmanuel Masanja ambaye ni mkazi wa kijiji cha Beledi aliishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuwapelekea mradi katika kijiji chao.
Alisema kwa muda mrefu wamekuwa wakiyafuata na kuyachota maji umbali mrefu ambaye pia wanauziwa hivyo kupitia Mradi wa EBARR watapata ahueni na kufanya shughuli za kujenga taifa kwa ufanisi.
Naibu Mkuu Dkt. Mkama yuko katika ziara ya kutembelea miradi ya EBARR ambapo wilayani Kishapu amekagua kiwanda kidogo cha bidhaa za ngozi Kijiji cha Kiloleli, malambo katika vijiji vya Kiloleli, Mihama na Beledi.
Miradi mingine ni ujenzi wa kituo cha kunenepeshea mifugo katika Kijiji cha Muguda, ujenzi wa majosho mawili katika vijiji vya Mihama na Muguda pamoja na kutembelea kaya zinazotumia majiko banifu.