Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima ameitaka Taasisi ya Chama cha Wanawake wafanya Biashara Tanzania (Tanzania Women Chamber Of Commerce-TWCC), kuhakikisha inakuwa mstari wa mbele na kuwafikia wanawake walioko vijijini ambao wamekuwa wakipitwa na fursa mbalimbali kutokana na mazingira yao hali inayo dumaza jitihada za kumkomboa mwanamke.
Dkt. Gwajima, ameyasema hayo jijini Dar es Salaam, Juni, 09, 2022 wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya ushiriki wa Makundi Maalum kwenye Manunuzi ya Umma shughuli iliyoandaliwa na taasisi ya Chama hicho.
Dkt. Gwajima ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imekuwa Mstari wa Mbele kuandaa mazingira wezeshi ya kumkomboa Mwanamke lakini fursa nyingi zimekuwa zikibakia kwa wachache waliopo mijini na kundi kubwa ambalo linafikia asilimia kubwa ya uzalishaji mali katika shughuli za kilimo wakibakia bila kuwa na taarifa sahihi.
“Niwaombe ndugu zangu wa TWCC, kwakuwa ninyi tayari mnamtandao mpana uliopo nchi nzima, mtumie fursa hiyo kuwafikia wanawake waliowengi ambao wapo maeneo ya vijijini hawa bado fursa nyingi hawazifahamu hivyo mkitumia vizuri jukwa lenu la TWCC, naimani wengi watapata mwamko na kushiriki katika mambo mbali mbali mathalani haya ya zabuni” amesema Dkt. Gwajima.
Dkt. Gwajima ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya kuwezesha Wanawake kiuchumi, aidha uwepo wa mifuko rasmi ya uwezeshwaji kiuchumi ikiwemo Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF), TASAF, Mfuko wa Rais wa Uwezeshaji na mifuko mingine ni ishara kuwa Serikali inawajali.
Dkt. Gwajima amesema kuwa mwaka 2016 Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya Mwaka ya Mwaka 2011 katika Kifungu cha 64 (a) katika kipengele cha 2 kwa kutoa nafasi kwa makundi maalum kuwezeshwa kushiriki katika fursa za manunuzi ya umma iliyotaka kutengwa asilimia thelathini (30%) ya bajeti yake kwa ajili ya makundi maalum wakiwepo wanawake.
Awali akizungumza kwenye Uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Taasisi ya Biashara ya Wananwake Tanzania Mercy Sila ameipongeza Serikali na kuomba jitihada hizo ziongezwe kwani wanawake walio wengi wanachukua mikopo wakiwa hawana maarifa ya Biashara au Shughuli wanayotaka kuifanya na hivyo kuishia kufilisika.
“Mhe Waziri pamoja na washiriki bado ipo changamoto kwa wanawake wanaochukua mikopo ikiwepo masharti yakukopa ambayo husisitiza kuwa kikundi cha watu jambo hili kwa namna moja linakwamisha jitihada za mtu mmoja mmoja, kwakuwa kila mtu anakuwa na mawazo tofauti hivyo hata wakichukua Mikopo wanashindwa kuelewana, lakini kama masharti yatabadilika itawezesha kila mwenye wazo lake ataweza kufanya anachoweza" alisema Sila.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum Khadija Shaaban Taya amesema wao kama wabunge wangependa kusikia zaidi sauti kutoka kwa Wanawake wenyewe juu ya yale yanayowasibu ili kwakutumia jukwaa la Bunge waweze kuwa na chakusema wakiwa Bungeni
“Nimpongeze sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Wizara lakini kutupatia Waziri Dkt. Gwajima ambaye amekuwa kila kukicha ni mtu wa kutafuta matokeo, hivyo lazima tumuunge mkono lakini na sisi wabunge kwa nafasi zetu mtuambie tuwe na cha kusema tuwapo Bungeni”. alisema Mhe.
Khadija
Ushiriki wa Wanawake kwenye Fursa za manunuzi ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Wanawake na Jinsia ya Mwaka 2000 na Mkakati wake wa utekelezaji wa mwaka 2005.