Mkuu wa Mkoa wa Mara, Mhe. Ally Hapi amesema uvuvi haramu unaoendelea katika Ziwa Viktoria hususan katika Mkoa wa Mara unachangiwa na baadhi ya Maafisa Uvuvi wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wavuvi haramu kuendeleza vitendo hivyo.
Hapi ameyasema hayo wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega aliyoifanya Mkoani humo.
Amesema kuwa wanazo taarifa za baadhi ya maafisa uvuvi ambao wanajihusisha na vitendo vya uvuvi haramu na ndio maana hata wanapoandaa operesheni hazifanikiwi kwa sababu wao ndio wamekuwa sehemu ya kuvujisha taarifa.
"Mhe. Naibu Waziri hapa ninayo majina kadhaa ambayo yamekuwa yakijirudiarudia ya maafisa wanaotuhumiwa kushiriki vitendo vya uvuvi haramu, nikuahidi kuwa tunakwenda kuchukua hatua kali dhidi ya wote watakaobainika kwa ushahidi wa wazi", amesema Hapi
Kufuatia tuhuma hizo, Mkuu huyo wa Mkoa amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa huo kuhakikisha ndani ya wiki tatu anafanya ufuatiliaji na kutathmini maafisa uvuvi wanaolalamikiwa na awasilishe taarifa kwake ili aweze kuchukua hatua za kunusuru sekta ya uvuvi.