Mhe. Mchengerwa- kila la heri Serengeti Girls kombe la dunia



Na John Mapepele

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitaka  Timu ya  Soka ya Wanawake chini ya umri wa miaka  17 ( Serengeti Girls) leo Mei 23, 2022 kucheza kufa na kupona dhidi ya Cameroon ili kujihakikishia  kucheza kombe la dunia.

Mhe. Mchengerwa ametoa kauli hiyo leo ikiwa ni masaa machache kabla ya Serengeti Girls kushuka dimbani nchini Cameroon leo jioni kwa majira ya saa  11: 30 ya hapa nchini.

Amesema watanzania wanamatumaini makubwa na wanaiombea timu hiyo ili kwa mara ya kwanza katika historia  ya mchezo wa soka Tanzania ishiriki katika mashindano ya dunia ambayo yanatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu nchini India.


Ameongeza kuwa ili kufuzu kucheza kombe la dunia  Serengeti Girls imebakiza  kucheza na kushinda mechi mbili tu  kwa maana ya mechi ya leo na ile ya marudiano itakayochezwa Juni 4, 2022 Zanzibar.

Aidha amesema mafanikio haya yanapatikana sasa kutokana na mapenzi ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwenye michezo ambapo ametoa fedha nyingi kusaidia timu zote za taifa katika michezo mbalimbali ili ziweze kufanya vizuri na kuipeperusha bendera ya Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.



" Hapa naomba  nitoe shukrani na pongezi za dhati kwa Rais wetu mpendwa, kwa  mapenzi makubwa na sapoti kubwa anayotoa kwenye michezo ambayo imeleta mapinduzi makubwa" amesisitiza Mhe. Mchengerwa

Pia amefafanua kuwa kwa mara ya kwanza Timu ya Taifa ya Soka kwa  Watu wenye Ulemavu ( Tembo Warriors) inakwenda kushiriki kombe la dunia Oktoba mwaka huu nchini Uturuki.
Previous Post Next Post