Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu mwelekeo wake kwa siku za usoni kuwa ni pamoja na kutumia ndege isiyo na rubani kufanya tafiti za kina ili kuboresha shughuli hizo kwa lengo la kupata matokeo yenye tija zaidi.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba wakati akitoa mada kwa kamati hiyo katika Semina iliyofanyika ukumbi wa AbdulKarim Mruma- GST , jijini Dodoma na kuhudhuriwa na wajumbe wa kamati hiyo pamoja na viongozi waandamizi kutoka wizarani.
Ameongeza kuwa, kutokana na ukuaji wa tekinolojia duniani ikiwemo mahitaji ya sasa ya madini ya viwandani na kulingana na utajiri wa rasilimali madini ambayo nchi ya Tanzania imejaliwa kuwa nazo, mweleko wa GST ni kufanya tafiti kwa kutumia njia hiyo ili kuyafikia maeneo mengi na kwa haraka.
Aidha, Dkt. Budeba ametaja mwelekeo mwingine wa GST kuwa ni kufanya uchorongaji wa kimkakati ili kupata taarifa za uhakika za madini, kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine zilizo chini ya wizara ikiwemo Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) pamoja na kuhakikisha inafungua Ofisi za GST kwenye Kanda ili kuigawa jiolojia kuwawezesha wachimbaji wadogo na wadau wengine kupata huduma katika kanda hizo kwa uharaka.
Pia, Dkt. Budeba amesema kuwa taasisi hiyo iko kwenye hatua za mwisho za kukamilisha maandalizi ya utoaji kitabu cha madini ya viwandani yanayopatikana nchini ambayo yanahitajika sana kwenye soko la dunia ambapo kitabu hicho kitawawezesha wadau kujua maeneo ya uwekezaji.
Kwa niaba ya Meneja Ukaguzi wa madini na Uchunguzi, Mhandisi Priscus Kaspana ameieleza kamati kuwa, GST imepanga kusogeza huduma za maabara kwa wateja kwenye mikoa na kanda mbalimbali na kwa kuanzia, itaanza na Mkoa wa Geita lengo likiwa ni kupanua wigo wa utoaji huduma za GST.


