Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumbu Tanzania, Brigedia Jenerali Hashim Komba akizungumza na waandishi wa Habari, ametaja na kuelezea baadhi mafanikio makubwa waliopata katika Shirika la Nyumbu tangu likipoanzishwa mwaka 1977.
Baada ya kuzungumza na Waandishi wa Habarii, Brigedia Jenerali Hashim Komba pia aliwatembeza waandishi kwenda kujionea mitambo mbalimbali na vitu walivyovifanya Shirika hilo.
Ifuatayo ni baadhi ya Miradi iliyoanzishwa na inayofanywa na Shirika la Nyumbu
Mradi wa Mtambo wa Kufyatulia Matofali
Shirika la Nyumbu limeunda mtambo wa kufyatulia matofali ya udongo wa mfinyanzi na sementi kidogo sementi (powered inter--ocking brick making machine). Mtambo huu huzalisha matofali ya bei nafuu yasiyohitaji kuunganishwa kwa wakati wa ujenzi.
Aidha gharama ya mtambo huu ni ndogo ikilinganishwa na mitambo mingine inayofanana
nayo ambayo huagizwa kutoka nje ya nchi. Kwa sasa Shirika linauza mashine hii kwa Tsh 14.5 Milioni ukilinganisha na zinazoagizwa kutoka nje kwa bei ya Tsh 25 Milioni. Uwezo wake ni kutengeneza tofali 120 kwa saa kwa lita moja ya Mafuta ya Diesel. Mtambo huu tayari unatumika katika baadhi ya halmashauri za wilaya na miji kama vile Misungwi, Mbinga, Handeni na Mtwara, pamoja na makampuni na watu binafsi.
Mtambo umesaidia sana katika kuongeza kasi ya kujenga makazi na majengo mbalimbali kwa ajili ya utoaji huduma kwa jamii kama vile; madarasa, zahanati, masoko na nyumba za kuishi kwa
bei nafuu. Mradi huu unaunga mkono juhudi za serikali katika sera yake ya kuleta maisha
bora kwa kila mtanzania kwa kujenga nyumba zenye gharama nafuu pamoja na kuleta ajira
kwa vijana wetu. Mpaka sasa Shirika limeuza ni zaidi ya mashine 90.
Mradi wa Kusindika Nyuzi Ndefu za Mkonge (Mobile Sisal Decorticator) kwa ajili ya Wakulima Wadogowadogo
Pia shirika hilo limebuni na kuunda mtambo wa kusindika mkonge unaozalisha nyuzi ndefu kwa ajili ya matumizi ya wakulima wadogo wadogo.
Mashine hii, ambayo inaweza kuhamishwa kutoka shamba moja hadi jingine, ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wadogo wadogo wa zao la mkonge ambao kwa muda mrefu wamekuwa hawawezi kuendeleza kilimo chao kutokana na gharama kubwa ya kusindika mkonge wanaozalisha kwa kutumia mitambo ya wakulima wakubwa (CORONA).
Aidha, mashine hii ina uwezo wa kuzalisha nyuzi za mkonge zenye ubora wa hali ya
juu na pia gharama yake ya manunuzi na uendeshaji ni nafuu ukilinganisha na mitambo
inayofanana nayo inayotoka nje ya nchi. Kwa sasa Shirika linauza mashine hii kwa Tsh 18
Milloni ukilinganisha na zinazoagizwa kutoka nje kwa bei ya Tsh 24.5 Milioni. Mradi huu
Uulikuwa unaunga mkono juhudi za serikali za kutekeleza sera ya Kukuza kilimo.
Mradi wa Kusindika Nyuzi Fupi za Mkonge kwa ajili ya kuzalisha Karatasi Maalumu
Shirika la Nyumbu chini ya ufadhili wa "United Nations Industrial Development Organization" (UNIDO), lilizalisha na kusimika mtambo wa kusindika nyuzi (singa) fupi za mkonge ambazo hutumika katika uzalishaji wa karatasi maalum kwa matumizi ya kutengeneza noti za Fedhana karatasi maalum za kuandaa mikataba. Mtambo huo umesimikwa katika mashamba ya Hale yanayomilikiwa na Kampuni ya Katani Ltd iliyoko
Tanga.
Mtambo huu umesaidia sana katika mipango ya Serikali ya kuendeleza zao la mkonge nchini
kwa kulipatia matumizi mbadala ya nyuzi ndefu na hivyo kuongeza mchango wa zao hili katika uchumi wa taifa.
Mradi wa kuzalisha Gesi kwa ajili ya kuzalisha Umeme
Shirika la Nyumbu kwa kushirikiana na kampuni ya ABM Equipment Services ya Ujerumani pamoja na kampuni ya Qingdao Tianren Environmental Engineering Co. Ltd ya Jamhuri ya Watu wa China lilijenga na kusimika mtambo wa kuzalisha gesi (biogas plant) inayotokana na makapi ya majani ya mkonge inayotumika kuzalisha umeme katika
mashamba ya Hale yanayomilikiwa na Katani Ltd.
Mtambo huu pamoja na ule wa kusindika nyuzi fupi za mkonge ulizinduliwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Jakaya Mrisho Kikwete mwaka 2008.
Mradi wa Mtambo wa Kutengeneza Mkaa Kutoka Kwenye taka za majumbani
Utunzaji wa mazingira umekuwa ni tatizo kubwa katika miji yetu kwa kukosa mfumo mzuri wa usombaji na uteketezaji wa taka zinazozalishwa majumbani. Sababu hii kubwa ndiyo iliyopelekea Shirika kubuni mtambo wa kutengeneza mkaa kutoka kwenye taka za majumbani ili kuwaokoa wananchi na athari zinazoweza kujitokeza
kutokana na mlundikano wa taka kwenye maeneo ya makazi. Mradi kwa kiasi kikubwa unalenga kwenye kuhifadhi mazingira pamoja na kupunguza ukataji miti hovyo hali inayotishia nchi yetu kuwa jangwa.
Mradi utasaidia sana katika nyanja za familia kutengeneza chanzo cha kuzalisha moto kwa ajili ya matumizi ya nyumbani bila kutumia gharama za ziada za kununua mkaa unaozalishwa porini, umeme au mafuta ambayo kwa ujumla gharama yake ni kubwa sana. Gharama ya mashine hii ni Tsh 11M.
Mradi wa Mtambo wa Kutengeneza Mkaa Kutoka Kwenye vumbi la makaa ya mawe
Mradi kwa kiasi kikubwa unalenga kwenye kuhifadhi mazingira pamoja na kupunguza ukataji miti hovyo hali inayotishia nchi yetu kuwa jangwa.
Mradi utasaidia sana katika nyanja za familia kutengeneza chanzo cha kuzalisha moto
kwa ajili ya matumizi ya nyumbani bila kutumia gharama za ziada za kununua mkaa unaozalishwa porini, umeme au mafuta ambayo kwa ujumla gharama yake ni kubwa sana. Gharama ya mashine hii ni Tsh 12.5M.
Hii ni baadhi tu ya miradi ambayo imefanya na inafanywa na shirika hili.



